BIASHARA
ya maduka ya dawa baridi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
imeingia shubiri, huku maduka mengine katika hospitali za Serikali
yakitakiwa kuwa tayari baada ya agizo la Rais John Magufuli, kuanza
kutekelezwa.
Dk
Magufuli alipoingia madarakani tu, moja ya maagizo yake alitaka Bohari
ya Dawa (MSD) kufungua maduka ya dawa za Serikali kwenye hospitali za
rufaa na za kanda, ambapo kesho kutwa Jumatatu duka hilo litaanza
kufanya kazi Muhimbili na bei za dawa zitakuwa chini ya bei ya soko.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laureane
Bwanakunu, amesema kufunguliwa kwa duka hilo kutaenda sambamba na
kufunguliwa na duka lingine katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya na
baadaye kwenye hospitali zingine za rufaa na kanda na yatatoa huduma
mpaka kwa wanaotumia utaratibu wa bima ya afya.
Kwa
mujibu wa Bwanakunu, pia MSD imeanza kuweka nembo ya Serikali kwenye
vidonge na hadi sasa ina vidonge 45 ambavyo vimewekewa nembo ya GOT, ili
kudhibiti wizi wa dawa za Serikali.
Bwanakunu
amesema agizo la Rais la kuitaka MSD kuanzisha maduka ya dawa karibu na
hospitali hasa pale Muhimbili, limekuja wakati muafaka.
Alisema
kwenye mpango mkakati wa miaka sita wa MSD, walikuwa na malengo ya
kufungua maduka hayo kwa ajili ya kusogeza huduma karibu kabisa na
wananchi.
“Agizo
la Rais limetekelezwa na duka la Muhimbili litafunguliwa Jumatatu,
tunamalizia hatua zilizobaki na mafundi wanafanya kazi usiku na mchana,” alisema na kuongeza kuwa duka hilo ambalo litatumia mfumo wa risiti wa kielektroniki, tayari vibali vyake vyote vimepatikana.
Bwanakunu
alisema wamefanya ziara ya kutembelea hospitali ya Benjamini Mkapa
iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kufanya mazungumzo na Naibu
Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Profesa Gesase Peter, ambaye aliahidi
kuwapa eneo kubwa kwa ajili ya kuendeshea duka hilo, litakalohudumia
wateja wa Kanda ya Kati.
Mkurugenzi
huyo alisisitiza kuwa maduka ya MSD ambayo yatafunguliwa kwenye
hospitali za rufaa na kanda, yatafanya kazi saa 24 na kuuza dawa na
vifaa tiba chini ya bei ya soko na yatahudumia watu binafsi na wale
waliopo kwenye taratibu za bima za afya.
Alisema
maduka hayo yataiongezea bohari wigo wa utendaji katika kutoa huduma
kwa wananchi, tofauti na sasa ambapo huduma ya dawa na vifaa tiba
zinatolewa kupitia mali zinazohifadhiwa katika bohari kupitia orodha ya
taifa ya dawa na vifaa tiba yenye aina ya dawa na vifaa tiba takribani
3,000 zinazoingizwa kwa mahitaji maalumu.
Kuhusu
udhibiti wa wizi wa dawa, Mkurugenzi huyo alisema MSD inafanya kazi za
uagizaji, uhifadhi na usambazaji kwa kutumia mfumo wa mtandao wa E9.
“Lakini
ili kudhibiti upotevu wa dawa za Serikali tangu mwaka wa fedha uliopita
tumeanza kuziwekea alama ya GOT bidhaa zetu ikiwa ni pamoja na vidonge,
mkumbuke zamani ilikuwa tunaweka kwenye vifungashio vya ndani na
maboksi alama ya MSD, lakini sasa hata kidonge kina alama ya GOT, pale
Dar es Salaam nina sampuli ya vidonge hivyo,” alisema.
Alisema
vidonge ambavyo tayari vimewekewa nembo ya GOT vipo 45 na wanaendelea
kuwapa maelekezo wazabuni, ili vyote viwekwe alama hizo.
Akitaja
aina za dawa zenye nembo ya serikali, Mkurugenzi huyo alisema tayari
dawa aina ya Diclofenac, Amoxillin, Ciprofloxacin, Contrimoxale,
paracetamol na magnesium.
Pia
alisema sasa wataanzisha huduma ya kutoa taarifa kwa njia ya simu ili
wananchi watakapoona kuna wizi wa dawa za Serikali, watoe taarifa na
wananchi wataelimishwa kutoa taarifa pale wanapoona dawa za serikali
mitaani.
“Dawa
nyingi zinaibwa kwenye vituo ambavyo dawa zinapelekwa na sasa watatumia
mfumo wa kompyuta kubaini wizi wa dawa ambazo zimekuwa zikiibwa mkoa
moja na kupelekwa mkoa mwingine.
“Rais Magufuli amesema miongoni mwa vipaumbele vyake ni maji na dawa, MSD imejipanga kuokoa maisha ya Watanzania,” alisema na kuongeza kuwa bajeti ya dawa ikiongezwa na kufikia Sh bilioni 250 kila mtu atapata dawa.
0 comments:
Post a Comment