Ndugu
zangu, muda huu nimeona kwenye mitandao kadhaa watu wakifurahia hatua
ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ndugu yetu Paul Makonda kutoa amri
(ambayo imetekelezwa) ya kuwaweka ndani wataalam wa ardhi ambao
walishindwa kufika eneo la kazi kwa wakati.
Binafsi
siungi mkono kitendo cha watendaji kuchelewa maeneo ya kazi lakini
zaidi ya yote siungi mkono kitendo cha mkuu wa wilaya kuwaweka ndani
watendaji kwa kosa la kuchelewa kazini.
Madhara
ya kuwachekea wakuu wa wilaya pale wanapotoa amri zinazokiuka haki za
msingi za wafanyakazi ni makubwa mno. Huko nyuma tulizoea mambo haya
kufanywa na wakuu wa wilaya enzi za Nyerere, hatutarajii hadi leo wakuu
hawa kuendesha wilaya zao kwa amri.
Ni
muhimu sana masuala ya kazi yaendeshwe kwa sheria na kanuni za kazi na
huyo mtu anayefurahia mamlaka (haramu) ya ma DC kuweka watu ndani
atakuwa na matatizo makubwa. Watu wanapaswa kuwekwa ndani kama wamefanya
makosa kwa mujibu wa sheria na si kama apendavyo DC.
Tuijenge
nchi yetu kimfumo zaidi kuliko ki-amri, nchi zinazoendeshwa kwa amri
amri huwa hazifiki kokote, kama tutashindwa kujijenga kimfumo katika
miaka hii mitano tukategemea kuendesha nchi kwa amri, matamko na mikwara
- ikifika 2020 tutaulizana nini kilifanyika na sote tutabaki kusimulia
matamko lukuki yaliyotolewa.
Nimalizie
tena kwa kuwakumbusha kuwa "Afrika itajengwa na mifumo imara, watu
imara hawawezi kuijenga Afrika maana siku moja watakufa, na kama
watakufa bila kuacha mifumo imara - yale yote waliyoyafanya yatapotea
haraka ".
Ndugu
yetu DC, Paul Makonda, tujengeeni mfumo imara utakaofanya wafanyakazi
wote kuwa kazini kwa wakati, (msijijenge ninyi) watu imara na amri
lukuki!
Mtatiro J.
0 comments:
Post a Comment