Gavana
wa Jimbo la Siaya, nchini Kenya, Cornel Rasanga ameingia matatani
akidaiwa kutumia Sh20 milioni za nchi hiyo (karibu Sh400 milioni) kutoka
katika mfuko za Serikali kwa ajili safari ya kuhudhuria sherehe za
kumwapisha Rais John Magufuli.
Dk
Magufuli alipishwa Novemba 5, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam
baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mshindi wa uchaguzi
wa urais uliofanyika Oktoba 25.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kenya (PAC), Nicholas Gumbo
amemtuhumu Rasanga kwa kutumia fedha hizo kutoka kwenye mfuko wa
Serikali wa safari.
“Gavana
wa Rasanga lazima awaambie wananchi wa Siaya, imekuwaje akatumia Sh20
milioni kwenda Tanzania kwa ajili ya shughuli ya Dk Magufuli?
“Sidhani
kama Dk Magufuli ana uhusiano wowote na wananchi wa Kaunti ya Siaya
kiasi cha Gavana kutumia fedha hizo za umma kwenda Tanzania,” alisema
Gumbo.
Gumbo
alisema Dk Magufuli anafahamika kuwa ni rafiki mkubwa wa kiongozi wa
Cord, Raila Odinga ambaye pia alihudhuria sherehe hizo.
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wa Afrika.
Akizungumzia
tuhuma hizo, Rasanga alisema madai yalitolewa na Gumbo ambaye ni Mbunge
wa Rarieda, ni uzushi na alikuwa anataka kujikweza kisiasa.
“Hii ilikuwa safari binafsi. Hatukutumia fedha za Serikali kama inavyoelezwa,” alisema alipohojiwa na gazeti la Daily Nation.
Gavana huyo alisema alikwenda kuhudhuria kuapishwa kwa Dk Magufuli kwa mwaliko binafsi wa Rais hiyo wa Tano wa Tanzania.
Hata hivyo, alisema ziara yake Tanzania itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza ushirikiano katika Ukanda wa Ziwa Victoria.
“Ukweli
ni kwamba Rais wa Tanzania aliwahi kutembelea Siaya na tulijadiliana
masuala mbalimbali ikiwamo usafiri hasa katika Ziwa Victoria,” alisema
Rasanga na kuongeza:
“Dk
Magufuli anatokea Kanda ya Ziwa na mpango wake mkubwa ni kuimarisha
bandari katika Ziwa Victoria na kuchaguliwa kwake kuwa Rais
kutarahisisha zaidi utekelezaji wa mipango yake.
“Hakuna
sababu ya kuingiza siasa katika safari hii. Tuko katika mipango mizuri
tu ya kibiashara na Tanzania ambayo kwa sasa imeanza kupanuka.”
Mwenyekiti huyo wa PAC Kenya alisema safari hiyo ya Novemba 5, ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Hata hivyo, Naibu Gavana, Wilson Ouma alipinga madai ya Gumbo akisema alikuwa na lengo la kumharibia bosi wake.
“Ukweli
Gavana Rasanga alitumia fedha zake kwenda Tanzania na uzushi wowote
unatakiwa ukomeshwe,” alisema Ouma alipozungumza na Nation.
Akisisitiza,
Gumbo alisema ataendelea kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma
unaofanywa na maofisa wa Serikali kwa kutumia vyeo vyao.
0 comments:
Post a Comment