Wakati
Rais John Magufuli akitarajiwa kuzindua na kulihutubia Bunge leo,
ametahadharishwa kutoambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
kwa maelezo kuwa si rais halali wa Zanzibar kikatiba.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema Zanzibar haina Rais, hivyo kiongozi huyo kushiriki Bunge kwa
nafasi hiyo ni kuvunja Katiba ya nchi.
Profesa
Lipumba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha CUF, ameungana na
msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walioutoa mjini Dodoma
juzi wakidai kuwa Dk Shein hapaswi kuingia kwenye ukumbi wa Bunge wakati
Rais Magufuli atakapohutubia.
Alishauri
endapo kuna ulazima wa Rais wa Zanzibar kuhudhuria, Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC) itangaze matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais wa Zanzibar na
rais aliyeshinda aapishwe.
Lipumba
pia amemtaka Rais Magufuli kutumia nafasi yake ya Amiri Jeshi Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania kuishauri ZEC kurejea matokeo
ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 na kumtangaza mshindi.
“Wazanzibari hawawezi kuruhusu uchaguzi kurudiwa, ” alisema Lipumba.
Alisema
anashangazwa na hatua ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuondoka
madarakani na kumwachia Magufuli mgogoro wa Zanzibar. Alisema Kikwete
alipaswa kuhakikisha matokeo yanatangazwa na mshindi anaapishwa.
Alisema
Kikwete alipoingia madarakani alionyesha kusononeshwa na mgogoro wa
Zanzibar na kuahidi kuupatia ufumbuzi wa kudumu lakini inashangaza kuona
akiondoka madarakani huku kukiwa na mgogoro mkubwa.
“Ninamuomba
Rais Magufuli asilifumbie macho suala hili, awaeleze wenzake wa CCM
waache kumuwekea vikwazo katika kipindi chake hiki cha kuliongoza
Taifa,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema
kuiminya demokrasia Zanzibar ni kuwapa fursa watu wenye itikadi kali
kuwashawishi Wazanzibari hasa vijana kuamini kuwa hawawezi kupata haki
kwa kupitia sanduku la kura.
Alisema
endapo kauli ya Wazanzibari kupitia kura zao haitaheshimiwa, wananchi
wake watapoteza imani kuwa hawawezi kupata mabadiliko kwa njia ya
kidemokrasia.
“Hili
ni jambo la hatari sana, si kwa Wazanzibari pekee, bali kwa Watanzania
wote na ukanda mzima wa Afrika Mashariki…tusijenge mazingira ya kuwapa
fursa watu wanaotaka mabadiliko kwa njia haramu,” alisema Lipumba.
Alisema
kitendo cha CCM kukataa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar kinaweza
kuliingiza Taifa kwenye mgogoro wa kisiasa na kiusalama, Magufuli akatae
kupelekwa huko,” alisema Profesa Lipumba.
Akizungumzia
mtazamo wake juu ya Serikali ya Magufuli, Profesa Lipumba alisema
ameanza vizuri kwa kutamka nia yake ya kudhibiti matumizi mabaya ya
fedha za umma kwa kupiga marufuku safari za nje.
Alisema hatua hiyo ni ishara kuwa ataweza kuwatumikia Watanzania kwa moyo.
Alimtaka
Rais Magufuli kutekeleza dhamiri yake ya kupambana na ufisadi kwa
kuwafungulia mashtaka na kuwafunga wote waliochota fedha katika akaunti
ya Tegeta Escrow.
0 comments:
Post a Comment