Eda
Malick kutoka Tanzania Women and Children Welfare center akizungumza na
waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia
Afande
Christina Onyango, Afisa wa Polisi, mkoa wa kipolisi Ilala akielezea
namna ambavyo dawati la jinsia wamejipanga kufikisha ujumbe wa siku 16
za kupinga ukatili wa kijinsia.
Waandishi
wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini Tanzania wakihudhuria mkutano
na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia.
Bahati
Mandago kutoka shirika la Tanzania Human Rights fountain akielezea
mikakati ya shirika lake katika kufikisha ujumbe wa Funguka. Chukua
Hatua Mlinde Mtoto apate elimu.
Wadau
kutoka katika mashirika mbalimbali wanaoshiriki kikamilifu katika
utekelezaji wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari
Dr.
Judith Odunga Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF akisoma taarifa kwa
vyombo vya habari kuhusiana na kuanza kwa siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia.
FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU
Katika kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kuanzia
tarehe 25 Novemba mpaka 10 Desemba, WiLDAF, Mashirika ya Haki za Binadamu,
Wadau wa Maendeleo na Asasi za Kiraia watatoa elimu na kuhamasisha umma
kuchukua hatua kumlinda mtoto ili apate elimu bora na salama. Ulinzi wa mtoto ni
pamoja na kuzuia vitendo vyote vya ukatili
wa kijinsia.
Maadhismisho ya SIku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia mwaka
huu yanalenga zaidi kuzungumzia suala zima la usalama mashuleni, lengo kuu ikiwa kuhamasisha umma
kuhusu ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia kwa vijana na watoto wetu
mashuleni, kwani vitendo vingi vya ukatili wa kijinsa vimekuwa vikiripotiwa.
Utafiti uliyofanywa na Chuo cha Tiba Cha Muhimbili (MUHAS)
kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika,
(WiLDAF) umetambua hatari zinazochangia ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na
wazazi kutowajali watoto na kutoa adhabu kali kwao na hivyo kuwafanya watoto
kuwa na hofu. Wakati mwingine watoto kufanyiwa ukatili bila wao kufahamu. Aidha,
adhabu ya viboko inahusishwa kama moja ya aina za ukatili dhidi ya watoto. Hii
inaathiri maendeleo ya elimu ya watoto katika taifa letu.
Kukosekana kwa usawa kati ya watoto wa kiume na wa kike hunapelekea
kuwajengea hofu watoto wa kike, na wakati
huo kuwajengea watoto wa kiume ujasiri wa kuona kuwa ni sahihi kwao kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aidha, tafiti kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto (VAC) uliofanywa
na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) wa mwaka 2011 ulionesha
kwamba watoto 3 wa kike kati ya 10 na mtoto 1 kati ya watoto 7 wa kiume wenye
umri kati ya miaka 13-24 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kingono. Aidha, asilimia
6 ya watoto wa kike wamelazimishwa kufanya tendo la ngono kabla ya miaka 18.
Pia utafiti huo unaonesha kuwa watoto wa kike wanafanyiwa vitendo vya kingono na wanaume waliowazidi umri wakati watoto wa
kiume wanafanyiwa ukatili na watoto wenye umri sawa.
Tafiti pia imeonesha kuwa vitendo hivyo vinafanywa na watu
wanaowafahamu wakiwemo majirani, wapenzi wao, watu wenye mamlaka (walimu). Ni asilimia 32.2 tu ya watoto wa kike na
asilimia 16.6 ya watoto wa kiume wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na
watu wasiofahamika na watoto. Vitendo hivi hufanyika maeneo ambayo uangalizi wa
watu wazima unahitajika kuwepo kwa mfano mashuleni, njiani, majumbani na wakati
mwingine katika vyombo vya usafiri.
Ni dhahiri kwamba kwa mazingira, mila na utamaduni
ikijumuisha familia za Kitanzania, vimekuwa vikichangia vitendo vya ukatili wa
kijinsia. Vitendo vya ukatili na udhalilishaji vina madhara makubwa ya kiafya kwa
watoto kwani hukatisha uwezo wao wa kielimu, mahudhurio ya shule na hivyo
kupelekea matokeo mabaya ya katika
ufaulu wao wakati wa mitihani.
Aidha, mazingira yasiyo salama kwa watoto wa shule yana madhara
makubwa. Watoto wanapokuwa mashuleni na kufanyiwa ukatili wa kingono wapo
katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya UKIMWI kwa mathlani mara tatu
zaidi ya wale ambao hawajawahi kufanyiwa ukatili.
Tunaamini kwamba kuondolewa kwa vikwazo vinavyo chochea
ukatili wa kijinsia kwa watoto wa shule kutachangia katika kuleta usawa wa
kijinsia kwa watoto wa kiume na wa kike. Pia mazingira mazuri ya shule yatasaidia
mahudhurio mazuri ya watoto mashuleni na kuleta matokeo mazuri katika ufaulu.
Jamii inahaswa kuweka mazingira mazuri ya shule ikiwa ni
pamoja na kuwepo miundombinu kama mabweni, vyoo, madawati, uzio kuzunguka
mashule na vyombo rafiki vya usafiri. Haya yote yatawezekana tu ikiwa kutakuwa
na dhamira ya dhati kwa watunga sera, wazazi, walimu, wanafunzi na jamii kwa
ujumla katika kuzuia ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto. Kuna haja
ya makusudi kabisakutofumbia macho
masuala ya ukatili kwa ujumla wake ili kujenga jamii imara.
Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia ni tukio la kimataifa la kila mwaka ili kuwa
na nguvu ya pamoja katika kuzuia kuenea
kwa janga hili . Ndani ya siku hizi, kuna siku zingine muhimu za kimataifa ,
mathlani, Novemba 25 ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake,
Novemba 29 ni Siku ya Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Binadamu, Desemba 1 ni
Siku ya UKIMWI Duniani, Desemba 3 ni Siku ya Kimataifa ya watu wenye Ulemavu,
Desemba 6 ni Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Mauaji ya kikatili ya Montreal
1989, ambapo wanawake 14 waliuawa na mtu aliyekuwa anawachukia wanawake. Tarehe
hizi zilichaguliwa mahususi ili kuhusianisha kwamba ukatili wa kijinsia unaongeza
maambukizi ya UKIMWI na ni Ukiukwaji wa Haki za Binadamu.
Katika kipindi hiki cha Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili
wa Kijinsia , mamia ya asasi za kiraia na wadau mbalimbali Tanzania wataifikia
jamii kwa kauli mbiu inayosema;
FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU.
Kauli hii inalenga kumshawishi mtu binafsi, kuwashawishi
walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla, kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha kwamba
shule ni mahala salama. Ni vema kutafakari kwa kina jinsi vitendo vya ukatili
wa kijinsia mashuleni vinavyoathiri maendeleo ya watoto wetu kielimu. Hivyo na
haja ya kuwa na taifa linalopiga vita vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.
Taifa linalofumbia macho ukatili wa kijinsia
haliwezi kupiga hatua kimaendeleo.
Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia ina lengo
la kushawishi watunga sera, wadau na jamii kwa ujumla, kuchukua hatua dhidi ya
ukatili wa kijinsia . Pia ina taka jamii kufichua vitendo vyote vya ukatili wa
kijinsia ili kuwa na jamii isiyovumilia
ukatili wa aina yoyote.
Hivyo basi WiLDAF na wadau mbalimbali wanaopinga vitendo vya
ukatili wa kijinsia wanaitaka serikali kufanya yafuatayo;
1) Kufutwa kwa adhabu ya viboko mashuleni
na walimu kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala.
2) Kutengeneza muongozo wa utekelezaji
wa sera ya elimu ya mwaka 2014
utakaolekeza upatikanaji wa elimu ya msingi iliyo bora na salama.
3) Kuboresha miundo mbinu rafiki kwa
watoto wa shule ikiwa ni pamoja na
kuwepo kwa vyoo bora, mabweni, madawati, usafiri, uzio kuzunguka shule
na mengineyo kwa ustawi wa watoto wa shule.
4) Kuunda mabaraza yatakayokuwa
yanasimamia malalamiko ya wanafunzi mashuleni.
5) Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa
kushirikiana na Wizara ya sheria na Katiba zitunge sheria ya kudhibiti Ukatili
Majumbani na kubadilisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971inayoruhusu mtoto wa kike
chini ya miaka 18 kuolewa, ama kwa ridhaa ya wazazi, mlezi au Mahakama.
Katika kipindi hiki cha siku 16, za kupinga ukatili wa
kijinsia kutakuwa na shughuli mbalimbali na midahalo ili kuleta mabadiliko
katika nchi yetu. Tunatoa wito kwa jamii kwa ujumla kupaza sauti na kukemea
vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Jamii ihamasishe usawa wa kijinsia,
mahusiano yasiyo na ukatili na isibague au
kunyanyapaa waathirika wa ukatili wa kijinsia. Tusikae kimya bali tufichue
ukatili wa kijinsia na kuchukua hatua kuwalinda watoto wetu iliwapate elimu
bora na iliyo salama. Kwa pamoja kupitia kauli mbiu ya mwaka tunasisitiza;
FUNGUKA! CHUKUA HATUA
MLINDE MTOTO APATE ELIMU.
Imefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani
(USAID Tanzania)
Imetolewa na;
Dkt. Judith N. Odunga (MKURUGENZI)
Kwa niaba ya:
Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani
Afrika (WiLDAF)
S.L.P 76215
DAR ES SALAAM
0 comments:
Post a Comment