Uongozi wa hospitali ya Rufaa
Bugando jijini Mwanza, umelaani matumizi mabaya ya mabomu ya machozi
yaliyofanywa na jeshi la polisi mkoani Mwanza kwa lengo la kuwatawanya
wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo ( Chadema ) ndani ya
hospitali hiyo na kusababisha taharuki kubwa kwa baadhi ya wagonjwa
pamoja na watumishi wa hospitali hiyo.
Mkurugenzi
mkuu wa hospitali hiyo Prof. Kien Mteta amesema kitendo cha jeshi la
polisi kufyatua mabomu ya machozi katika eneo la chumba cha kuhifadhia
maiti kimewatia hofu wagonjwa na wauguzi na kuongeza kuwa amesikitishwa
kuona ugomvi wa kisiasa ukihamia ndani ya hospitali hiyo na kwamba
tayari ameijulisha wizara ya afya na ustawi wa jamii kuhusu kadhia hiyo
pamoja na kuliwasilisha kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza.
Kamanda
wa polisi mkoa wa Mwanza, naibu kamishna Charles Mkumbo anasema askari
polisi hawakuwa na namna nyingine ya kumuokoa askari mwenzao, mkaguzi
msaidizi wa polisi wilayani Geita Ngasa Joseph, zaidi ya kuwatawanya
wafuasi wa Chadema kwa mabomu wakati walipokuwa wakimshambulia na
kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake.
0 comments:
Post a Comment