MBUNGE
Mteule wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi ameanza kuikumbuka jamii
anayoiongoza kwa kutoa fedha taslimu na bidhaa mbalimbali kwa wanafunzi
walemavu wanaosoma shule ya msingi mchanganyiko Makalala ya mjini Mafinga.
Bidhaa
hizo
ni pamoja na mafuta kwa ajili ya albino, na miwani, dawa za meno,
sukari,
sabuni, shampoo, fagio, pipi, mikate, biskuti na Sh 100,000
zitakazotumika kununua nguo za ndani za watoto 23 walemavu wanaosoma
shuleni hapo.
Akikabidhi
bidhaa hizo kwa wanafunzi hao, Chumi alisema; “badala ya kuchinja mbuzi na kula
na timu yangu ya kama wanavyofanya wengine katika kusheherekea ushindi wao, mie
nimeingia kazini, tuwakumbuka watoto hao na tukaamua kuchangishana na kununua
vitu hivi vichache kwa ajili yao.”
Chumi
alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo jipya mkoani Iringa kwa kupata kura 18,379
dhidi ya kura 12,834 alizopata mshindani wake wa jirani, William Mungai wa
Chadema na kura 208 za mgombea wa ACT Wazalendo, Mwangiri Mwangiri.
“Nimeanza
kwa kuwakumbuka watoto hawa walemavu wa shule hii, nitaendelea kufanya hivyo
kwao na kwa wengine kila ninapopata fursa ya kuchangia mahitaji yao. Kazi hiyo
itakwenda sambamba na kusimamia utekelezaji wa Ilani yetu ya CCM ili zile ahadi
zetu zote tulizoahidi wakati wa kampeni zitekelezwe,” alisema.
Chumi
alisema jimbo la Mafinga Mjini lina fursa nyingi za kiuchumi ambazo kama
zitatumika vizuri zitasaidia kupunguza changamoto mbalimbali za kimaendeleo
zinazowakabili watu wa jimbo hilo.
Kwa
upande wake aliyekuwa kampeni meneja wa mbunge huyo mteule, Albert Chalamila
aliutaka uongozi wa shule hiyo kwa kushirikiana na timu Chumi, kuandika andiko
la mradi na kuliuza kwa wafadhili ili wasaidie maendeleo ya wanafunzi walemavu
wanaosoma shuleni hapo.
Akishukuru
kwa
msaada huo, Mkuu wa shule hiyo, Shem Muheni alisema; "msaada huu
unawaongezea faraja wanafunzi hawa kama mnavyowaona wamefurahishwa na
hivi vyote mlivyowaletea na kila mmoja anataka apate."
Alisema
wanafunzi hao wanaotoka katika mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe, Iringa na Morogoro
wanahitaji misaada wa hali na mali kutoka katika makundi mbalimbali ya jamii ili
kukamilisha pale panaposhindwa kukamilishwa na serikali kwa wakati muafaka.
“Watoto
hawa wana mahitaji mengi, na baadhi yake ni ya gharama kubwa, kwahiyo ni jambo
la kheri pale wadau mbalimbali wa maendeleo wanapojitokeza na kuwasaidia ili
nao waweze kukamilisha ndoto zao za kupata elimu wanayoihitaji,” alisema na kumshukuru Chumi kwa msaada huo.
Muheni
alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 ilianza kwa kupokea wanafunzi
wasioona mwaka 1974 kabla ya kuanza kuchukua watoto wenye mtindio wa ubongo na
walemavu wengine miaka iliyofuata.
0 comments:
Post a Comment