Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka makatibu tawala wa mikoa nchini
kuchukua hatua kali dhidi ya wote waliosababisha kuwapo kwa watumishi
hewa.
Amesema suala hilo la watumishi hewa limeisababishia
Serikali hasara kubwa, hivyo ni lazima watu wote waliohusika katika sakata hilo
wabainishwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Majaliwa
alisema hayo jana alipokuwa akipokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa
Lindi iliyowasilishwa na mkuu wa mkoa huo, Godfrey Zambi katika siku ya
kwanza ya ziara yake ya pili kikazi wilayani Ruangwa.
Wakati akiwaapisha
wakuu wapya wa mikoa Machi 15, Rais John Magufuli aliwapa siku 15
kuhakikisha wanabaini watumishi hewa wote katika mikoa yao na kuwaondoa
katika mfumo wa malipo.
Baada ya kufanyika kwa kazi hiyo, jumla
ya watumishi hewa 7,795 walibainika ambao wameisababishia Serikali
hasara ya Sh7.5 bilioni.
Awali, Zambi alisema Lindi ina jumla ya
wafanyakazi watoro 57 na hewa saba ambao walifariki na wengine
kustaafu, lakini walikuwa wakilipwa mishahara na kuisababishia Serikali
hasara ya Sh36 milioni kwa mwezi.
0 comments:
Post a Comment