Milio ya risasi ilirindima juzi na kuzua tafrani wakati Mahakama ya
Wilaya ya Bukombe ilipohamia mahabusu ya ngo’mbe kuhakiki idadi ya mfugo
iliyokamatwa ndani ya Hifadhi ya Mdendeli Muowisi Kigosi, mkoani Geita.
Inadaiwa
kuwa risasi hizo zilizokuwa zikifyatuliwa na watu wasiojulikana
zililenga kuwatisha waliokuwa wakiendelea na kazi ya uhakiki iliyokuwa
ikisimamiwa na Hakimu Gabriel Kurwijila na kulindwa na askari 35
mahakamani wa idara ya wanyamapori.
Katika tuko hilo, askari 10
walilazimika kujibu mapigo na kufanya eneo hilo kugeuzwa uwanja wa vita.
Baada ya askari wanyamapori na polisi kufanikiwa kuwafurusha wavamizi, walitokomea porini kabla ya kutiwa mbaroni.
Kazi hiyo iliendelea na kubaini ng’ombe wote 454 wana afya njema ndipo Hakimu Kurwijila alipoahirisha shauri hilo.
Hata
hivyo, uhakiki huo ulibaini uwapo wa ng’ombe wa ziada 139 ambao kwa
mujibu wa Wakili wa Serikali Mwasimba Hezron, inawezekana waliwafuata
wenzao wanaolindwa na askari wa wanyamapori.
Kutokana na hofu ya
kuvamiwa wakiwa njiani kurejea Ushirombo, Hakimu Kurwijila aliamuru
askari wanyamapori na polisi kuimarisha ulinzi kuhakikisha wote walioko
kwenye msafara wanafika salama.
Kesi hiyo inawakabili washtakiwa watano wanaodaiwa kukutwa wakichunga mifungo ndani ya eneo la hifadhi kinyume cha sheria.
Washtakiwa hao leo wanaanza kujitetea na wanatarajiwa kuitwa mashahidi sita kupinga ushahidi wa upande wa mashtaka.
Washtakiwa hao ni Emanuel Wapi, Musa Manyakenda, John Wapi, Nkwabi Ngeleja na Masan Makura.
0 comments:
Post a Comment