Kamati
maalumu ya uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda imefichua madudu na harufu ya ufisadi katika utekelezwaji wa
mikataba mitatu, inayohusu maeneo ya ukusanyaji mapato ya Stendi Kuu ya
Mabasi Yaendayo Mikoani ya Ubungo na kodi ya uegeshaji magari katikati
ya mji.
Kutokana
na madudu hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha wazi kuwa hataki kufanya
kazi tena na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe na Kaimu
wake, Sarah Yohana na kuwasilisha majina yao kwa mamlaka husika ya
nidhamu kwa hatua zaidi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema hivi karibuni
aliunda kamati hiyo maalumu kufuatilia maeneo hayo muhimu kutokana na
malalamiko ya muda mrefu, ambayo ofisi yake ilikuwa ikipokea kutoka kwa
wananchi.
Alisema
kwa mujibu wa uchunguzi, kamati hiyo ilibaini kuwa katika stendi ya
mabasi ya Ubungo, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma,
ikiwemo kutokuwasilishwa kwa mapato halisi yanayotokana na makusanyo ya
kila siku serikalini.
“Kamati
ile imebaini kuwa pale ubungo kunatumika sheria ndogo mbili za
ukusanyaji mapato moja ya mwaka 2004 na nyingine mwaka 2009 kwa lengo la
kunufaisha wachache,” alisema Makonda.
Alifafanua
kuwa Sheria Ndogo ya Mwaka 2004 ya ukusanyaji mapato ndani ya kituo
hicho, inaonesha kuwa kila basi linatakiwa kutozwa Sh 4,000, hivyo
makusanyo halisi kwa mwezi ni Sh milioni 42 kutokana na mabasi 350
yanayoegeshwa kituoni hapo.
Hata
hivyo, alisema kutokana na mabadiliko ya tozo, sheria hiyo
ilibadilishwa mwaka 2009 na kila basi likawa linatozwa Sh 8,000 na hivyo
makusanyo ya mwezi yakapanda na kufikia Sh milioni 82 kwa mwezi.
“Lakini
cha kushangaza tumebaini kuwa bado kampuni inayokusanya mapato katika
kituo cha Ubungo, inawasilisha mapato hayo kwa kutumia sheria ya mwaka
2004 yaani Sh milioni 42 badala ya Sh milioni 82 kwa mwezi…”
“…Mbaya
zaidi kamati ile katika ukaguzi wake, ilikuta kampuni ya ukusanyaji
mapato hayo stendi ya Ubungo inayo Sheria ya Mwaka 2009 lakini katika
nyaraka za Halmashauri ya Jiji zinaonesha sheria inayotumika ni ya mwaka
2004,” alisisitiza Makonda.
Alisema
katika uchunguzi ilibainika kuwa kampuni iliyo chini ya Halmashauri ya
Jiji inayokusanya mapato hayo stendi ya Ubungo, ilisaini mkataba wa
ukusanyaji mapato hayo kwa mara ya kwanza Januari 31, 2004 na baadaye
ikasaini tena mkataba Januari 30, mwaka jana.
Kwa
mujibu wa Makonda, kwa hali ilivyo tangu Sheria Ndogo ya Mwaka 2009
ipitishwe, haijawahi kutumika na hivyo kulisababishia hasara jiji hilo
ya Sh bilioni tatu kutokana na mapato katika stendi hiyo kuendelea
kuwasilishwa kwa kutumia sheria ya mwaka 2004.
“Ukipiga
hesabu za harakaharaka utagundua kuwa kila mwezi Sh milioni 42 zimekuwa
zikipotelea kwenye mikono ya wachache, kwa maana hiyo kuanzia mwaka
2009 Sh bilioni tatu zimepotea na kila mwaka tumekuwa tukipoteza Sh
milioni 500, huu ni ufisadi wa aina yake kwa kweli,” alisema.
Alisema
wakati fedha hizo zikipotea kwenye mikono ya wachache, kamati hiyo pia
ilibaini kuwa hali ni mbaya katika kituo hicho cha Ubungo kwani pamoja
na ukosefu wa vyoo na maegesho bora kwa mabasi, lakini pia vibanda vya
biashara vilivyomo ndani ya stendi hiyo, vimekuwa vikitumika kukandamiza
maskini na kunufaisha wachache.
“Kwa
mujibu wa taratibu, kila kibanda mle ndani ya stendi kinatakiwa
kukodishwa kwa Sh 200,000 kwa mwezi, lakini tumebaini kuwa wapo watu
wachache wamevihodhi na kuvikodisha kwa zaidi ya Sh milioni 1.5,” alisema.
Kuhusu
mkataba wa maegesho katikati ya jiji kupitia Kampuni ya National
Parking System (NPS), alisema kamati hiyo pia imebaini kuwa Halmashauri
ya Jiji imeiongezea mkataba wa miezi 10 kampuni hiyo kinyume cha
taratibu wakati mkataba wake ulikuwa umeshamalizika.
Alisema
mara baada ya mkataba huo kumalizika Agosti mwaka jana Mkurugenzi wa
Jiji, Kabwe aliiandikia barua kampuni hiyo na kuiongezea muda wa miezi
sita kwa madai kuwa mchakato wa kutafuta mzabuni mpya pamoja na kwamba
umeanza, haujakamilika.
Aidha,
Kaimu Mkurugenzi Yohana naye aliandika miezi kadhaa baadaye barua na
kuiongezea tena kampuni hiyo muda wa miezi minne iendelee kukusanya kodi
ya maegesho kwa kuwa bado mchakato wa kutafuta mzabuni mpya
haujakamilika.
“Barua
zote mbili zina saini ya viongozi hawa wawili, hatua hizi ni kinyume
kabisa na maadili ya viongozi pamoja na Katiba ya nchi. Haiwezekani
mchakato wa kumtafuta zabuni uchukue zaidi ya miezi sita,” alieleza Makonda.
Pamoja
na hayo, Makonda pia alisema kamati hiyo katika uchunguzi wake dhidi ya
Kampuni ya Tambaza inayosimamia makosa ya pikipiki na maegesho ya
magari katika sehemu zisizotakiwa, imekuwa ikitoza fedha nyingi za faini
kinyume cha mkataba.
“Mkataba
wao unaonesha wazi kuwa wanatakiwa wakikamata pikipiki yenye makosa
watoze faini ya Sh 20,000 lakini imebainika wao wanatoza zaidi ya Sh
80,000. Licha hivyo pia mkataba unawataka wazingatie dharura na
kutotumia lugha chafu lakini yote haya hawayazingatii,” alisema.
Alisema
tangu Rais John Magufuli aingie madarakani amekuwa mstari wa mbele
kupiga vita ubadhirifu wa fedha za umma, rushwa na ufisadi hivyo akiwa
kama Msaidizi wa Rais anaunga mkono juhudi hizo ndio maana hawezi
kunyamazia madudu yeoyote yanayohusu ufisadi.
“Nimewasiliana
na mamlaka husika ya nidhamu ili ichukue hatua stahiki dhidi ya
viongozi hawa wawili Kabwe na Yohana na nimeiambia mamlaka hii kwa uwazi
kabisa siwahitaji kuendelea nao hapa Dar es Salaam,” alisisitiza.
Aidha,
alisema tayari amewasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) kuhusu mikataba hiyo yote mitatu ambayo imeahidi kuanza
kuifanyia kazi leo.
Alisema
ameamua kuchukua hatua hiyo ya kuwashughulikia wakurugenzi hao kwa kuwa
wao ndio tatizo kwani mikataba hiyo hata ikivunjwa kwa sasa itakuwa ni
kazi bure kama viongozi hao wataendelea kuwepo.
Hii
ni mara ya pili kwa Stendi ya Ubungo kuingia katika kashfa ya
ubadhirifu wa fedha, ambapo mwaka 2011, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo
Pinda aliagiza ufanyike uchunguzi, uliobaini kuwepo kwa madudu, hali
iliyosababisha mzabuni aliyekuwepo kuondolewa.
0 comments:
Post a Comment