Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Amani Mkwizu na mfanyakazi wa
kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart, Edward Magobela wamepandishwa
kortini jana wakikabiliwa na mashtaka matatu ya rushwa.
Washtakiwa
hao walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakidaiwa kuomba rushwa ya Sh50 milioni na nyingine ya Sh5 milioni na
kupokea Sh3 milioni kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Commercial Sales
and Services
Tanzania Limited, Glenn Clarke.
Akiwasomea mashtaka yao, Wakili wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Denis Lekayo alidai
washtakiwa hao waliomba na kupokea kiasi hicho cha fedha ili kumwezesha
mkurugenzi huyo kupunguziwa kodi aliyokuwa anadaiwa kutoka Sh375
milioni hadi Sh100 milion.
Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashtaka na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu
Huruma Shaidi anayesikiliza kesi hiyo, aliwaeleza washtakiwa hao kuwa
dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili. Hata
hivyo, walishindwa kutimiza masharti na kupelekwa mahabusu.
Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 9 mwaka huu.
Awali,
akiwasomea mashtaka, Wakili Lekayo alidai kuwa washtakiwa walitenda
makosa hayo Aprili 19, mwaka huu, jijini Dar es Salaam kinyume cha
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Namba 7 ya mwaka 2011.
Katika
shtaka la kwanza, Wakili Lekayo alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja na
wengine ambao hawajakamatwa, waliomba rushwa Sh50 milioni kutoka kwa
Clarke.
Wakili Lekayo, alidai katika shtaka la pili washtakiwa hao
kwa pamoja na wengine ambao hawajakamatwa bado, walijihusisha na vitendo
vya kumuomba rushwa ya Sh5 milioni mkurugenzi huyo ili wampunguzie kodi
kutoka Sh375 milioni mpaka Sh100 milioni.
Katika Shtaka la tatu,
Wakili Lekayo alidai washtakiwa kwa pamoja walijihusisha na vitendo vya
rushwa kwa kupokea rushwa ya Sh3 milioni kutoka kwa Clarke ili
wampunguzie kodi kutoka Sh375 milioni mpaka Sh100 milioni.
0 comments:
Post a Comment