Wataalamu wa kuandaa mitaala
ya elimu wametakiwa kuzingatia viwango vya soko la ajira katika kuandaa mitaala
itakayotumika kufundishia shuleni na vyuoni.
Rai
hiyo imetolewa na mratibu wa uendelezaji wa mitaala na mkufunzi kutoka
chuo cha ualimu ufundi stadi veta Morogoro, Julias Mwakasasa wakati wa mafunzo
ya kuandaa mtaala wa masomo ya misitu uliondaliwa na taasisi binafsi ya Private
Forestry Programme (Panda miti Kibiashara) ya mjini Iringa.
Mwakasasa alisema kuwa ili kutoa elimu ya misitu kikamilifu, mtaala wa awali wa masomo ya misitu unahitaji kuandaliwa kwa kutegemea soko ambalo litaendana na mahataji ya sasa katika mazao ya misitu katika soko la ajira.
Alisema kuwa kwa kuzingatia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika nchi ya Tanzania na dunia kwa ujumla mahitaji mbalimbali yamezingatiwa katika maandalizi ya mtaala ambapo umewashikirisha wadau mbalimbali nchini wanaojishughulisha katika mazao ya misitu.
Alisema asilimia kubwa ya soko la sasa linahitaji wataalamu watendaji zaidi katika kufanya kazi hivyo mtaala utakaondaliwa kwa ajili ya wanafunzi wa awali wa misitu utazingatia vigezo vinavyohitajika katika soko la sasa katika utendaji zaidi.
“Mitaala inahitaji kuwa na uwezo wa kujenga ari ya kujielimisha na utashi wa kuendelea kutafuta maarifa na stadi za kiutendaji zaidi kuliko kukaa tu ofisini ambapo wataalamu wengi wamekuwa wakitegemea kutoa maelekezo wa wafanyakazi ambao hawana elimu ya misitu.
Aliongeza kuwa upatikanaji wa wa mazao ya misitu utamsaidia mwanafunzi kuamua na kufikiri zaidi ya mawanda ya ufahamu uliotolewa kwa kutoa mawazo mapya na kujenga dhana mpya katika uvunaji na uzalishaji wa misitu.
Kwa upande wake Katibu wa Wamiliki wa Viwanda vya Mbao (Safia), Wiliam Mgowole alisema kuwa Mtaala huo ukikamilika unatarajiwa kumwezesha mwanafunzi kupata ujuzi zaidi katika mazao ya misitu na kuwezesha uzalishaji wa kitaalamu wa mbao utakaoendana na soko.
Alisema kuwa kutokana na wafanyakazi wengi kukosa elimu hiyo wamekuwa wakipoteza asilimia zaidi ya 70 ya mazao ya mbao kutokana na kutokuwa na wataalamu katika viwanda vya uzalishaji mbao.
Naye ofisa Misitu mkuu wa Msitu wa Taifa (Sao Hill), Salehe Bereko alisema wadau wa misitu wataweza kupata taaluma sahihi na kuongeza uzalishaji na kutosheleza mahitaji ya soko la ndani na nje.
Alisema
kutokana na kupungua kwa mgao wa uchakataji wa mazao ya misitu kutoka meta za
ujazo milioni moja mpaka 600,000 kwa mwaka upandani wa miti kitaalamu na
matumizi ya teknolojia ya kisasa inayopunguza upotevu wa mazao wakati wa
uchakataji ndio njia sahihi ya kukamiliana na changamoto hiyo.
0 comments:
Post a Comment