Thursday, April 14, 2016

Mkapa, Kardinali Pengo Wammwagia SIFA Rais Magufuli

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amesema viongozi wote wanawajibika kuishi kwa mfano wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Sokoine aliyejitoa kutumikia taifa huku akimtaja Rais John Magufuli ametokana na kuishi namna hiyo.

Alisema hayo juzi baada ya misa takatifu ya kumkumbuka Sokoine iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Rais John Magufuli.

Mkapa alisema mfano huo wa Sokoine, ndio ulioiwezesha Tanzania kumpata kiongozi wa sasa, Rais John Pombe Magufuli anayetaka kuonesha misingi ya uongozi bora, uadilifu, kusimamia amani, utulivu na maendeleo.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alimpongeza Rais Magufuli kwa kufuata nyayo za Sokoine katika kuliongoza Taifa.

Akizungumza kwenye misa hiyo, Kardinali Pengo alisema waliwasiliana na Dk Magufuli kwa simu wakati akiwa mapumzikoni Chato mkoani Geita na Rais alimueleza maneno ambayo yanaonyesha kuwa kazi ya urais si rahisi, na jinsi kiongozi huyo wa kiroho alivyompa moyo.

“Sijui ni vizuri nikisema Mheshimiwa Rais, lakini kwa vile uliyataja maneno hayohayo hata kule Chato. Napenda kusema yale uliyosema kwangu binafsi kwa njia ya simu,” alisema Kadinali Pengo.

“Ulisema ‘ningelijua kwamba kuwa Rais ndiyo hivi, wala nisingeligombea urais’ … na mimi nilisema afadhali mtu mmoja afe kuliko Taifa liteketee. Kwa hiyo endelea mbele.”

Kadinali Pengo, aliyeonekana awali kusita kuweka bayana mazungumzo hayo, alisema kwa kuwa Rais Magufuli alishaeleza hayo akiwa Chato, basi angependa aeleze sehemu ya mambo aliyowahi kuzungumza naye kwa simu.

Ingawa Kadinali Pengo hakueleza kile alichozungumza Rais akiwa Geita, Dk Magufuli amekuwa akieleza jinsi kazi ya urais ilivyo ngumu na kila mara kuomba wananchi wamuombee na kumsaidia kutekeleza majukumu yake.

Akiwa kwenye ibada iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria, Parokia ya Chato, Rais aliwataka Watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.

Kadinali Pengo alitoa dokezo hilo siku ya kukumbuka kifo cha Sokoine, ambaye amejijengea sifa ya kuwa mpambanaji katika vita dhidi ya uhujumu uchumi, uvivu, wizi wa fedha za umma na matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.

Alieleza katika misa hiyo kuwa watu wanamfananisha Rais Magufuli na waziri mkuu huyo wa tatu tangu nchi ipate uhuru.

Alisema kuna ming’ono kuwa sura ya Rais Magufuli inafanana na ya Sokoine, akisema maneno mengi ya mtaani ni ya ukweli zaidi ya yale yanayoandikwa na vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Rais Magufuli aliwasihi Watanzania kuendelea kushikamana, kupendana na kuenzi mazuri yaliyofanywa na viongozi wa taifa waliotangulia mbele ya haki, akiweno aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine.

Magufuli alihimiza Watanzania kuenzi mazuri yote yaliyofanywa na viongozi wengine waliotangulia mbele ya haki, hususani Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume, Magufuli alisema kazi nzuri ya mtu huwa haipotei.

Alisema anamkumbuka Sokoine alivyokuwa kiongozi shupavu, aliyewapenda watanzania, aliyependa kuwatumikia watanzania, mchapakazi, aliyechukia rushwa, aliyechukia ufisadi na aliyechukia uonevu kwa watu wa chini.

“Namuona (Sokoine) ni kielelezo cha pekee katika Taifa letu la Tanzania, miaka 32 iliyopita wakati Mzee wetu Edward Moringe Sokoine alipoitwa na kutangulia mbele ya haki, wakati huo mimi nilikuwa JKT Mpwapwa, ninaikumbuka siku hiyo ilikuwa ya majonzi makubwa,” alisema.

Sokoine alifariki dunia miaka 32 iliyopita, kwa ajali ya gari katika eneo la Dakawa wakati akitokea Bungeni Dodoma.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More