Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo tarehe 1/4/2016
imemfikisha Mahakamani Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa Mbunge wa Sumve
ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Mtaji na Uwekezaji kwa kosa la
kushawishi na kuomba Rushwa ya Shilingi Milioni thelathini
(30,000,000/-) kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11
ya mwaka 2007 kifungu cha 15 (i)(a) na (2).
Akiwa
kama mjumbe wa Kamati ya Mtaji na Uwekezaji tarehe 13/3/2016 Mhe.
Ndassa alimwomba rushwa ya shilingi Milioni 30 kutoka kwa Mtendaji Mkuu
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Felchesmi J. Mramba ili
amsaidie kuwashawishi wajumbe wengine wa Kamati ya Mtaji na Uwekezaji
kupitisha bila kipingamizi taarifa ya TANESCO kwa mwaka 2015/2016.
Mbunge
huyo amefunguliwa kesi namba 118/2016 na alisomewa mashtaka hayo na
Wakili wa TAKUKURU Dennis Lekayo akishirikiana na Emmanuel Jacob katika
Mahakama ya Kisutu mbele ya Mhe. Hakimu Emirius Mchauro.
Mshtakiwa
yupo nje kwa dhamana baada ya kupata mdhamini mmoja na kulipa shilingi
milioni 10. Uchunguzi wa shauri hili bado unaendelea na kesi hii
itatajwa tena tarehe 18/4/2016.
IMETOLEWA NA
OFISI YA AFISA UHUSIANO
TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA, MAKAO MAKUU
1 APRIL, 2016.
0 comments:
Post a Comment