Tuesday, April 12, 2016

Wachina Watatu Wahukumiwa kwa Kukwepa Kodi.

Raia watatu wa China wamehukumiwa kwenda jela kifungo cha miezi sita au kulipa faini ya Sh4 milioni kila mmoja, baada ya kukiri kukwepa kodi ya Sh350,000 kwa kutumia Mashine ya Kielektroniki (EFDs).

Washtakiwa hao ambao walifikishwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala ni Liu Songyue, Liu Pengfey na Jiang Zedong ambao ni wamiliki wa Kampuni ya M/S Sen He Co.Ltd.

Hata hivyo, washtakiwa hao walilipa faini hiyo na kuepa kwenda jela miezi sita.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Juma Hassan alisema washtakiwa hawana kumbukumbu ya makosa ya awali na kwamba, Sheria ya Kodi inaruhusu washtakiwa wenye makosa kama hayo kulipa faini, kifungo au vyote kwa pamoja.

Pia, Hakimu Hassan aliamuru kutolewa kwa hati ya kukamatwa mshtakiwa wa nne ambaye hakufika mahakamani.

Alisema kutokana na washtakiwa kukiri makosa yao, watatakiwa kulipa faini ya Sh4 milioni kila mmoja, au jela miezi sita. 

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Wakili wa washtakiwa, Nihimia Mkoko alidai washtakiwa wakilipa faini, wataendelea na shughuli zao na kulipa kodi vizuri kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Awali, Wakili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Marcel Busegano alidai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutoa taarifa za uongo kwa Kamishna.

Wakili Busegano alidai washtakiwa walitenda kosa hilo Machi 12 maeneo ya Tabata Shule, wilayani Ilala katika Kampuni ya M/S Sen He Co. Ltd.

 Alidai washtakiwa walitoa risiti ya mauzo kwa mteja, Mwise Wambura ya Sh200,000 kutoka kwenye mashine ya EFDs inayomilikiwa na kampuni hiyo.

Aliendelea kuwa siku hiyohiyo, maofisa wa TRA walitembelea eneo hilo kufanya ukaguzi na kugundua kuwa, walikwepa kodi kwa makusudi kwa kujifanya wamepokea kiwango hicho ilhali mteja alilipa Sh550,000.

Mshtakiwa wanne anatakiwa kufikishwa mahakamani hapo Mei 9.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More