Baadhi ya Wabunge wamehoji uhalali wa kisheria wa Rais John Magufuli
kuhamisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe ya Muungano na
kuzipeleka kwenye ujenzi wa barabara katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Wabunge
hao walihoji hilo wakati wa semina iliyofanyika jana katika Ofisi Ndogo
za Bunge jijini Dar es Salaam , iliyoendeshwa na Dk Haji Semboja kutoka Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam na Harold Sungusia wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC).
Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali alihoji juu
ya mamlaka ya Rais katika kutumia fedha ambazo zilishapangiwa bajeti na
Bunge na kuzipeleka kwenye maeneo mengine.
Alihoji
pia juu ya nidhamu ya Serikali katika usimamizi wa Bajeti iliyopitishwa
na Bunge. Mbunge huyo alisema dhana ya mgawanyo wa madaraka haipo kwa
sababu Serikali ina nguvu kuliko Bunge na Mahakama hivi sasa.
Alisisitiza kuwa nguvu hiyo ndiyo inayomfanya Rais afanye kitu chochote anachotaka.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Lucia Mlowe alisema moja ya majukumu ya Bunge ni
kuisimamia Serikali, lakini anashangaa kuona yenyewe ikilisimamia Bunge
katika mambo mbalimbali.
Alisema hata suala la Rais kuhamisha
fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe ya Muungano, ni
kuingilia madaraka ya Bunge, kwa sababu fedha hizo tayari zilikuwa
zimeidhinishwa kwa ajili ya matumizi hayo.
“Naomba kupata
ufafanuzi kutoka kwa wataalamu hapa, Rais ana mamlaka gani ya kuhamisha
fedha zilizotengwa kwa ajili ya jambo fulani? Pia, ni namna gani wabunge
tunaweza kuisimamia Serikali kama hamna uwiano kati ya mihimili hii
mitatu,” alihoji mbunge huyo.
Akijibu hoja hizo, Dk Semboja alisema Sheria ya Bajeti ya 2015, inampa mamlaka Rais kupeleka fedha katika eneo analoona inafaa.
Alisema
sheria hiyo inatoa sharti moja, kwamba Rais kupitia Waziri wa Fedha,
atatoa taarifa bungeni juu ya matumizi ya fedha hizo.
Dk Semboja
alisema mamlaka hayo yanatambuliwa pia katika Ibara ya 137 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano, hivyo Rais hajakosea kuhamisha fedha hizo kwenda
kujenga barabara isipokuwa taarifa ya matumizi itolewe bungeni hata kama
matumizi yanaonekana.
“Bunge lazima lifahamishwe kuhusu matumizi ya fedha hizo.Kama ni udhaifu wa kipengele hiki, basi unaanzia kwenye Katiba,” alisema Dk Semboja.
Pia,
Sungusia alisema, “Fedha ambazo Rais hawezi kuziingilia ni zile zilizo
kwenye consolidated fund (mfuko hodhi), nje ya hapo anaweza kufanya
lolote,” alisema mwanasheria huyo.
0 comments:
Post a Comment