Tuesday, April 19, 2016

MWAMOTO ATAKA MAJI YA MTO RUAHA MDOGO YAMALIZE TATIZO LA MAJI MJI WA ILULA


MBUNGE wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto akiongea neno mbele ya kamati ya maji


MBUNGE wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto ameiomba serikali kutumia maji ya mto Ruaha Mdogo kumaliza tatizo la muda mrefu la maji linaloukabili mji mdogo wa Ilula, wilayani Kilolo mkoani Iringa wenye wakazi zaidi ya 38,000.

Mto huo unaopita mjini Iringa ukijazwa na vyanzo mbalimbali vidogo vya maji vikiwemo vya wilayani Kilolo, upo zaidi ya kilomita 30 kutoka mji huo wa Ilula wenye kata tatu za Lugalo, Nyalumbu na Ilula yenyewe.

Mwamoto alitoa ombi hilo juzi wakati Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Iringa Mjini (IRUWASA) ikikabidhi kwa Mamlaka  ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ya Mji Mdogo Ilula, mradi mdogo wa maji yanayotumiwa na mji huo toka chanzo cha mto Idemle baada ya kusimamia ukarabati wake uliogharimu Sh Milioni 903.

“Ufumbuzi wa tatizo la maji katika mji mdogo wa Ilula ni kutumia maji ya Mto Ruaha Mdogo badala ya pendekezo la kutumia chanzo cha Mgombezi ambalo gharama zake ni kubwa,” Mwamoto alisema.

Alisema endapo serikali itaendelea na mpango wa kutumia chanzo cha Mgombezi wananchi wa Ilula wasitegemee kupata maji ndani ya kipindi kifupi kijacho.

“Kama tutang’ang’ania kutumia chanzo cha Mgombezi, inaweza kuichukua Ilula zaidi ya miaka 10 kupata huduma ya maji safi na salama, ombi langu tutumie chanzo cha mto Ruaha Mdogo kuleta maji Ilula, na nadhani hata gharama zake zinaweza kuwa ndogo,” alisema.

Akitoa taarifa ya ukarabati wa mradi wa maji wa chanzo cha mto Idemle, Mkurugenzi wa IRUWASA, Gilbert Kayange alisema; “baada ya ukarabati huo uliofanywa kati ya mwaka 2013 na 2015, chanzo hicho sasa kinazalisha mita za ujazo 940 kutoka mita za ujazo 600 zilizokuwa zikizalishwa awali wakati mahitaji kwa siku ni mita za ujazo 2,609.”

Ili kutatua tatizo la maji katika mji huo, Kayange alisema serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa chanzo cha Mgombezi ambao gharama yake inaelezwa kuwa ni zaidi ya Sh Bilioni 15.

“Tunaongelea suala la Mgombezi kwasababu mradi huo ulikwishasanifiwa, lakini hiyo haitufanyi wataalamu tusiendelee kutafuta vyanzo vingine mbadala vitakavyosaidia kukabiliana na changamoto ya maji katika mji wetu wa Ilula,” alisema.

Akizungumzia kazi zilizotekelezwa wakati wa ukarabati wa mradi huo wa chanzo cha Idemle, Kayange alizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na kukarabati kidaka maji katika mto Idemele, kukarabati tenki la kuhifadhi maji Mazombe na ujenzi wa vitolea hewa katika bomba kuu la usafirishaji na ukarabati wa njia ya usafirsiahaji maji wenye urefu wa kilomita 14.

Nyingine ni pamoja na ujenzi wa mabomba mapya ya kusambaza maji safi yenye urefu wa kilomita 16.7 ambayo hata hivyo yamekuwa yakihujumiwa kwa kutobolewa na watu wasiojulikana.

Mtendaji wa kijiji cha Mazombe, Joseph Nyoni alisema; “mambomba ya plastiki yamekuwa yakitobolewa nay ale ya chuma yamekuwa yakibondwa sehemu za maungio na kusababisha kuvuja na kupoteza maji mengi yanayotakiwa kwa matumizi ya wananchi.”

Nyoni alisema katika kukabiliana na changamoto hiyo, wamefanya mikutano ya hadhara ili kuwashirikisha wananchi kuwafichua waharibifu wa mitandao ya maji.

Mbunge wa Kilolo ameliomba jeshi la Polisi kuwasaidia kuwabaini watu hao ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa uharibifu huo.

Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Ilula, Enock Ngoinde amesema wanahitaji zaidi ya Sh Milioni moja kukarabati mabomba hayo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More