Tuesday, April 19, 2016

Sera Ya Rais Magufuli ya Kubana Matumizi Yawaliza Wafanyabiashara Dodoma

Sera ya Rais John Magufuli ya kubana matumizi serikalini imekuwa majanga kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma, huku wizara nazo zikionja cha moto. 

Katika kipindi hiki cha kuanza kwa mkutano wa Bunge la Bajeti, wafanyabiashara mkoani hapa wamelalamikia biashara kudorora tofauti na kipindi kilichopita. 

Biashara kubwa zinazofanywa wakati wa vikao vya Bunge ni vyumba vya kulala wageni, usafiri wa teksi, kumbi za mikutano na vyakula. 

Mkutano wa bajeti uliopita, vyumba vya kulala wageni katika mji wa Dodoma vilikuwa vimejaa hata kabla ya kuanza mkutano wa Bunge, lakini hali hiyo imekuwa tofauti baada ya jana karibu nyumba zote za kulala wageni kuwa na nafasi nyingi huku nyingine zikiwa hazina wageni kabisa.

Mkutano huo unaoanza leo kupitisha bajeti za wizara na Serikali Kuu, huwa na mjadala mkali na maofisa wa wizara kutoka vitengo mbalimbali husafiri kutoka Dar es Salaam na sehemu nyingine nchini kwa ajili ya kusaidia utoaji wa majibu na hoja zinazotoka kwa wabunge. 

Kutokana na hali hiyo hoteli, nyumba za kulala wageni hutegemewa kuwa zimeshachukuliwa hadi siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano rasmi na mji wa Dodoma huanza kushamiri kibiashara, lakini kutokana na sera ya ubanaji matumizi wa Serikali ya Dk Magufuli, mji huo umepooza kama hauna wageni. 

Hata baadhi ya mawaziri wameeleza kuwa hawatachukua maofisa wengi kutoka wizara wanazozisimamia kwa ajili ya kushughulikia makadirio ya matumizi ya wizara zao, watakapowasilisha ndani ya Bunge, kama ilivyokuwa katika Serikali zilizopita. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, January Makamba alisema wizara yake imepunguza kwa zaidi ya nusu ya maofisa wanaokwenda kuhudhuria vikao hivyo Dodoma. 

“Katika Bunge hili si zaidi ya maofisa 10 watakaohudhuria ambao ni waziri, katibu mkuu na naibu wake, wakurugenzi mazingira, muungano sera na mipango, mhasibu mkuu pamoja na mkurugenzi wa Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC),” alisema. 
       

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema ingawa wizara yake haijafika muda wa kupanga juu ya maofisa wangapi wanaostahili kuhudhuria vikao hivyo, lakini ni lazima wahakikishe wanapunguza idadi hiyo. 

“Lazima tuangalie umuhimu wa mtu kulingana na sekta yetu ya elimu hatutaweza kuja na watu kama ilivyozoeleka huko nyuma,” alisisitiza Profesa Ndalichako ambaye awali alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini (Necta). 

Katika kuonyesha hatua za ubanaji matumizi zimeanza kuuma katika mji wa Dodoma, mmoja wa wahudumu katika nyumba ya kulala wageni iliyopo eneo la Majengo Mapya ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema: “Mwaka huu hakuna biashara kabisa, hata waliopata watu ni wale ambao wamekuja kwa ajili ya maandalizi ya sherehe za Mei Mosi zinazofanyika kitaifa hapa Dodoma.” 

Alisema wageni wa vikao vya Bunge la Bajeti huomba nafasi siku tatu kabla ya kuanza kwa vikao, lakini mwaka huu hadi kufikia jana mchana hakuna watu walioonyesha kutaka nafasi katika nyumba hiyo. 

Wafanyabiashara wa saluni ambao nao wanategemea vikao vya Bunge kuongeza mapato yao, walisema hali ya kibiashara ni mbaya na kwamba ina tofauti kubwa na vikao vingine vilivyopita.

Hata bei ya vyakula katika masoko mbalimbali haijapanda kama ilivyokuwa wakati wa vikao vilivyopita, hali iliyokuwa inayowalazimu wakazi wa mji huo kufanya manunuzi wiki moja kabla ya vikao vya Bunge kuanza.

Pia, kwa upande wa wingi wa watu na magari kwenye mji huo hali imekuwa tofauti na vikao vilivyopita vya bajeti, ambavyo kulikuwa na idadi kubwa ya watu siku mbili kabla ya kuanza vikao. 

Kama ilivyo kawaida ya maandalizi ya Bunge, barabara za maeneo mbalimbali mjini hapa zimeanza kufanyiwa ukarabati kwa kuwekewa viraka kwenye maeneo yenye mashimo na usafi kwa kuondoa mchanga barabarani.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More