Ofisa
Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga, Anamaria Yondani ameeleza kuwa kipindi cha
miezi mitatu wamekamata wahamiaji haramu 283, huku kampuni binafsi
zikiongoza kwa kuajiri watu hao kinyume cha utaratibu.
Pia
alifafanua kuwa wahamiaji hao 111 walikuwa sio rasmi, 45 walifikishwa
mahakamani, saba walifungwa, 103 walifukuzwa nchini, 172 waliachiwa huru
na waliomaliza kifungo ni wanne.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Yondani alisema
kukamatwa kwa wahamiaji hao kumetokana na kufanya msako mbalimbali na
kutoa elimu ya dhana ya uhamiaji shirikishi katika makundi mbalimbali ya
kijamii.
Alisema
wamewakamata wahamiaji haramu hao 283 wengine wakiwa wameajiriwa kwenye
baadhi ya kampuni binafsi kinyume cha sheria na taratibu za nchi,
wakiwa wanatoka katika mataifa tofauti tofauti.
“Kipindi
cha miezi mitatu tumefanikiwa kukamata wahamiaji haramu 283 huku
kampuni binafsi zikiongoza kuwapatia ajira kinyume na taratibu, mimi
nilikuwa nawaomba wamiliki wa kampuni hata wanapokuwa na vibali vya
kisheria wahamiaji hao basi wawaingize katika ajira kwa kufuata
utaratibu na sheria za nchi,” alisema.
Alisema
wengi wa hao wana vibali vya kuishi, lakini anaingizwa kwenye ajira
kinyume cha taratibu na ndio wengi wao wamekamatwa kwa makosa hayo.
Wahamiaji
hao wanatoka nchi za Kenya, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo (DRC), Rwanda, Somalia, Ethiopia na China.
0 comments:
Post a Comment