Friday, July 22, 2016

JWTZ yasema wapo tayari kukabiliana na ugaidi Afrika

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema lipo tayari kukabiliana na ugaidi nchini na kwingineko barani Afrika. 

Kwa wiki mbili mfululizo, askari wa JWTZ waliungana na majeshi ya nchi nyingine nane kufanya mafunzo maalumu ya kukabiliana na ugaidi, biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji wa binadamu na uharamia. 

Akitoa tathmini, Mkurugenzi wa Mazoezi hayo, Brigedia Jenerali Yohana Mabongo alisema yameenda vizuri na askari wamepata fursa ya kufahamiana na kubadilishana uzoefu. 

“Tupo vizuri. Tunaweza kukabiliana na uhalifu wa kimataifa, ndani na nje ya Tanzania,” alisema Brigedia Jenerali Mabongo. 

Alifafanua kuwa awali askari walikuwa wanafanya kazi kiutamaduni wakiwa na lengo la kulinda mipaka kwa kutumia silaha nzito, lakini kutokana na kubadilika kwa tishio la usalama, majeshi mengi duniani yameona kuna haja ya kuwa na mbinu mbadala. 

“Kupambana na gaidi au mtuhumiwa wa dawa za kulevya hakuhitaji kifaru au mzinga. Majanga yanayoletwa na mapigano au mashambulizi ya kushtukiza huacha athari nyingi kwa jamii ambazo hustahili msaada. 

"Tutayafanya hayo yote hapa nchini au popote Umoja wa Afrika (AU) utakapoona kuna haja ya kufanya hivyo,” alisema. 

Mafunzo hayo yanayoshirikisha raia kutoka AU, Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na Shirika la Msalaba Mwekundu yanafadhiliwa na Tanzania na Marekani. 

Jana, Balozi mdogo wa Marekani nchini, Virginia Blazer alitembelea Chuo cha Mafunzo ya Kuimarisha Amani Tanzania (TPC) Kunduchi na kupokea ripoti ya utekelezaji.

Uganda, Djibouti na Ethiopia ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki mafunzo hayo. 

Kwa muda mrefu, Uganda inakabiliana na Joseph Kony anaeendesha mapigano ya kisasi kaskazini mwa taifa hilo na alipoulizwa juu ya mchango wa mafunzo hayo, Kiongozi wa askari wa Jeshi la Uganda (UPDF), Kanali Fred Twinamatsiko alisema jeshi hilo lipo tayari wakati wote, lakini kuna changamoto za kufanikisha suala hilo. 

“Utayari wa kisiasa ndiyo unaokosekana. Mara nyingi tumempiga Kony na kumuondoa alipokuwapo. Endapo wakubwa watakuwa tayari, UPDF inamuondoa muda wowote,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More