Sunday, July 31, 2016

BARABARA NI CHANGAMOTO KATIKA USAMBAZAJI WA MADAWA VIJIJI

 
 IMEBAINIKA kuwa ubovu wa miundo mbinu ya barabara, hasa  za vijijini ni changamoto kubwa inayowakabili bohari ya madawa (MSD) wakati wa kusambaza madawa katika vituo vya afya nchi.
 
Hali hiyo imebainishwa na Ofisa wa Huduma kwa wateja wa MSD mkoa wa Iringa, Henry Luanda wakati wa mkutano wa kujadili masuala ya afya kwa wilaya ya Iringa mradi unaotekelezwa na shirika la  TACOSODE kwa ufadhili wa watu wa marekani (USAID) na kufanyika katika ukumbi wa Valentine mjini hapa.
 
Luanda alisema kuwa hali hiyo inasababisha magari ya MSD kuharibika na wakati mwingine kushindwa kufikisha dawa vituoni kwa wakati hali inayopelekea dawa hizo kuchina (expire) zikiwa boharini MSD.
 

Aliongeza kuwa Changamoto za upatikanaji wa dawa za uzazi wa mpango katika vituo vya kutolea huduma za afya zinatokana na baadhi ya watendaji kutojua mahitaji halisi ya dawa za uzazi wa mpango katika kituo, zahanati au hospitali husika na hivyo kuagiza kiasi kidogo au kingi kuliko mahitaji.


Alisema kuwa changamoto nyingine wanayokumbana nao kama msd ni baadhi ya tabia ya Udokozi unaofanywa na watumishi wa sekta ya afya wasio waaminifu na kusababishia wananchi vijiji kukosa madawa hasa kina mama wajawazito.


Luanda alisema kuwa msd imeandaa mikakati ya kuboresha upatikanaji wa dawa za uzazi wa mpango katika vituo vya kutolea huduma ya Afya na kuongeza wigo wa utoaji huduma na kupanaua mipaka ya huduma  kwa watu au kampuni binafsi katika maeneo ya utengenezaji dawa, vifaa tiba na usambazaji.
 
Aidha alisema kuwa mkakati mwingine wa msd ni kuongeza uwezo wa miundo mbinu ya ikiwa ni pamoja na Kujenga maghala manne katika mikoa ya  Iringa, Mtwara, Tanga, Mwanza na Muleba ifikapo 2016 na pia kuongeza idadi ya magari ya usambazaji.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TACOSODE, Theofrida Kapinga alisema kuwa shirika hilo linatekeleza miradi mbalimbali na mojawapo ni ushirikishwaji wa jamii katika upatikanaji wa huduma za afya kwa kutoa nafasi kwa wananchi kuweza kujadili.
 
Alisema kuwa nafasi wanazopatiwa wananchi kwa ajili ya kuweza kuisimamia serikali katika halmashauri zake kutoa huduma ambazo zimeboreka za afya katika vituo vya afya na zahanati kadri ya ubora unaohitajika.
 
Kapinga alisema kuwa mkutano huo pia unatoa fursa ya kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya na kuadhiri kwa kiasi fulani upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa na kujadili makubaliano ya Abuja kuhusiana na serikali kutenga asilimia 15 ya bajeti katika afya.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More