Wednesday, February 24, 2016

Nape aagiza mkataba wa StarTimes na TBC Upitiwe Upya

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ameitaka Bodi mpya ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia upya mkataba wa StarTimes na shirika hilo.

Amesema kumekuwa na maneno kuhusu mkataba huo, hivyo bodi inapaswa kubainisha vifungu vya sheria ambavyo vitahitaji kufanyiwa marekebisho.

Akizungumza katika uzinduzi wa bodi mpya chini ya Mwenyekiti wake, Balozi Herbert Mrango, Nape alisema mapitio hayo yanaweza kufanyika ndani ya mwezi mmoja, kubaini mapungufu yaliyopo.

“Bodi hii inapokea majukumu yaliyoachwa na bodi iliyopita. Majukumu hayo ni pamoja na kupitia upya mkataba wa StarTimes na TBC kwani mkataba uliopo utaisha na utatakiwa kuwa na mkataba mpya,’’ alisema Nape.

Pia aliitaka bodi hiyo kuhakikisha kwamba baada ya miaka minne, TBC inajiendesha yenyewe kiuchumi kwa kuzingatia uwekezaji katika viwanja vyao.

Alisisitiza kuwa ni vyema bodi hiyo ikaangalia upya muundo wa shirika hilo na kwamba wawashirikishe wafanyakazi ili wajue nafasi zao.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More