Thursday, February 25, 2016

MH:WILIAM LUKUVI ATOA MSAADA WA PESA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO IDODI

Mbunge  wa  jimbo la Isimani Bw  Wiliam Lukuvi ambae ni  waziri wa Ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi (kulia) akimpa maelekezo mwenyekiti wa  kijiji cha Mapogolo baada ya kumkabidhi fedha  kiasi cha Tsh milioni 2 za  kulipa fidia  ya ardhi kwa  wananchi  watakaohamishiwa makazi mapya  kutoka  kitongoji  cha Kitanewa Idodi ambao  nyumba   zao zilisombwa na mafuriko
Lukuvi kushoto akiwa na mkuu  wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela katikati jana
Mkazi wa Kitanewa  akifurahia  baada ya Lukuvi kuwapatia misaada  mbali mbali
Mmoja  kati ya  wakazi wa KItanewa ambao walikubwa na mafuriko aliyepata  kusoma na  waziri Lukuvi darasa moja  shule ya msingi akimsikiliza mbunge  wake
Mkazi  wa Kitanewa akilalamika   kunyimwa msaada wa mahindi ya msaada wakati yeye ni mlemavu japo  si mlengwa wa msaada  huo wa waathirika  wa mafuriko
Lukuvi  akielezwa  jambo  na  mmoja kati ya  waathirika  wa mafuriko Idodi
Mkuu  wa wilaya ya  Iringa Richard Kasesela  akimweleza jambo mbunge Lukuvi
MKazi  wa  kitanewa Idodi akimpongeza mbunge  wake Lukuvi kwa kuwajali wananchi
Mkuu  wa wilaya ya  Iringa Richard Kasesela Katikati na kamati yake ya Ulinzi na usalama  wakitazama daraja la Iringa  -kuelekea hifadhi ya  Ruaha  ambalo awali lilikuwa halipitiki baada ya  kusombwa na mafuriko na  sasa linapitika


  Na MatukiodaimaBlog
MBUNGE  wa jimbo  la  Isimani  Bw Wiliam Lukuvi amewapa pole waathirika  wa mafuriko wa kata  ya Mapogolo tarafa ya  Idodi wilaya ya  Iringa mkoani Iringa kwa kuwakabidhi msaada  wa pesa  zaidi ya Tsh  milioni 9  kwa ajili ya kusaidia mahitaji  mbali mbali ikiwa ni pamoja  na  kurejesha  miundo mbinu  ya maji  safi  iliyoharibiwa na mafuriko.

Bw  Lukuvi  ambae  pia ni  waziri  wa Ardhi  ,nyumba na maendeleo ya makazi alikabidhi msaada  huo  jana  baada ya  kutembelea  waathirika  hao  waliopo kambi  ya Kitanewa pamoja na kutembelea eneo la barabara  ya kutoka Iringa  kuelekea hifadhi ya  Taifa ya Ruaha ambayo kwa   sasa imekarabatiwa baada ya  awali barabara   hiyo kukatika kutokana na mafuriko hayo , alisema   kuwa  lengo lake  kama mbunge  wa  jimbo   hilo la Isimani na  serikali ni kuona  wananchi  waliokumbwa na mafuriko   wanaendelea  kusaidiwa .

Alisema  kuwa  awali aliomba msaada  wa mahindi   tani 100  kutoka   serikali kwa ajili ya waathirika  hao  wa mafuriko Idodi na  Pawaga  ikiwa ni   pamoja na  kuwasaidia  msaada  wa  fedha   kiasi cha  zaidi ya Tsh milioni 3 kwa ajili ya  kuwawezesha  waathirika  hao  wa mafuriko   kupata mahitaji mengine kama mboga na  pesa ya  kusagia mahindi hayo .

Bw  Lukuvi alisema  kuwa kwa ajili ya kurejesha  huduma ya maji kijijini hapo  amewasaidia kiasi cha Tsh  miliobni 4 ambazo  wameomba  kwa ajili ya  kuboresha miundo mbinu  hiyo ,pia kiasi cha Tsh milioni 2 kwa  ajili ya kukiwezesha   kijiji kulipa fidia ya ardhi  kwa  wananchi waliotoa ardhi  yao kwa ajili ya wakazi wa kitongoji cha  Kitanewa ambao wanapaswa  kuhamishwa eneo  hilo la mafuriko la  kupewa makazi mapya .

" Waambieni   watu  wenye mashamba ambayo yatachukuliwa kwa ajili ya viwanja mwaka   huu  wavune mazao yao na  baada ya  hapo kila  mmoja  muweze  kumlipa  fidia ya  Tsh 200,000 na  baada ya  hapo waitini  wataalamu  wa ardhi  ili  waweze  kupima  viwanja na  mpanfgilio  mzuri  zaidi kwa  ajili ya makazi mapya .......pia nataka hata mashamba ya  kawaida  ya wananchi kupimwa  ili kupata hati za ardhi zitakazowawezesha  kutumia kupata mikopo ....ila  nitawaletea mashine za  kufyatulia tofari ambazo  unaweza  kuzijengea  bila  kuchoma "

Alisema kuwa  kwa  ajili ya  kuhamasisha ujenzi  wa  nyumba   bora mwananchi atakayekuwa  wa kwanza  kupandisha  jengo atamchangia bati japo kwa  sasa amekwisha  toa bati  zaidi ya 300 kwa  mkuu  wa wilaya ya  Iringa kwa ajili ya  waathirika   hao.

Bw  Lukuvi  pia  amewapongeza wadau  mbali mbali zikiwemo taasisi za dini ,watu  binafsi ,taasisi ya  kifedha pamoja na mifuko  ya  hifadhi  za  jamii  kwa  kujitolea  misaada  mbali mbali kwa ajili ya waathirika  wa mafuriko na  wagonjwa  wa Kipindupindu  Pawaga  .

Pamoja na  kuwashukuru wadau hao  Lukuvi  alimpongeza   waziri  Mkuu Kassim Majaliwa kwa    kuwatembelea waathirika  hao wa Mafuriko na  wale  wa Kipindupindu Pawaga .

Hata  hivyo  Lukuvi  alimpongeza  mkuu  wa wilaya ya  Iringa Bw Richard Kasesela na  viongozi wote  akiwemo mkuu  wa mkoa Amina Masenza kwa   kusimamia shughuli  mbali mbali  ikiwemo ya urejeshaji wa miundo mbinu ya barabara   iliyokuwa  imekatika katika barabara ya Iringa - Ruaha .

Katika  hatua  nyingine  Bw  Lukuvi aliagiza  serikali ya  kijiji cha Mapogolo kutowabagua  wananchi  katika  kugawa chakula   hicho  cha msaada na  kutaka  hata  ambao  si waathirika  wa mafuriko ambao  wana njaa wapewe  chakula   hicho  cha msaada kwa  waathirika wa mafuriko .
 
Wakati huo  huo Waziri Lukuvi  alisema  kuwa serikali inakusudia  kuijenga  barabara ya Iringa- kuelekea   hifadhi ya  Ruaha  kwa  kiwango cha  lami kama  mbavyo Rais Dr John Magufuli alivyoahidi wakati  wa kampeni kupitia ilani ya  uchaguzi ya CCM

Pia  kwa ajili ya  kuwafanya  wananchi  kunufaika watalii wanaotembelea hifadhi hiyo ya Ruaha Iringa alisema  tayari  jitihada za  kujenga viwanja  vidogo  vya ndege  nje ya  hifadhi ya  Ruaha  zimeanza na  kuwa  lengo la  serikali ni  kuwahamisha wafanyakazi  wanaoishi  ndani ya  hifadhi  hiyo na  kujumuika na  wananchi  nje ya  hifadhi ili  waweze  kupata mahitaji kama  wananchi  wengine.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More