WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku tabia ya baadhi ya viongozi
katika maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi
wakiwemo wauguzi bila ya kufuata taratibu.
Pia
amewataka wauguzi nchini kufanya kazi kwa weledi, uaminifu pamoja na
kufuata maadili ya taaluma yao kwa kuwa maisha ya wagonjwa yako chini
yao.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Oktoba 04, 2017) wakati akifungua
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 45 wa Chama cha Wauguzi Tanzania, mkoani
Lindi.
“Naagiza
viongozi wote kufuata na kuzingatia sheria. Kama kuna makosa ya
kitaaluma, Mabaraza husika yashughulikie jambo hilo na ni marufuku
kuwaweka ndani watumishi kwa tuhuma za kitaaluma.”
Amesema
kwamba katika sekta ya afya bila wauguzi ambao ni kundi kubwa kati ya
Wanataaluma wa Afya, Serikali haitaweza kutekeleza ipasavyo mikakati
mbalimbali iliyopangwa kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo.
Katia
hatua nyingine Waziri Mkuu amewaasa wauguzi wote nchini kuhakikisha
wanazingatia kiapo cha maadili ya kazi yao na kwamba Serikali
haitamvumilia yeyote atakae bainika kwenda kinyume.
“Nanyi
Wauguzi mnao wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kiapo
na miiko ya taaluma yenu. Tunazo taarifa kuhusu baadhi ya Wauguzi kutoa
lugha chafu kwa wagonjwa, kuomba rushwa na wengine kujihusisha na
vitendo vya wizi wa dawa.”
Amesema
lengo la Serikali ni kuhakikisha afya za Watanzania wote zinaimarika
ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya kuinua uchumi na
kufikia wa kiwango cha kati, hivyo ni lazima watoe huduma bora kwa
wananchi.
Pia
amewaomba waunge mkono kwa nguvu zote jitihada za Serikali katika
kuhakikisha miundombinu na vifaa vyote havihujumiwi na watu wachache ili
viwe msaada mkubwa hususani kwa akina mama wajawazito ili wajifungue
salama.
Akizungumzia
kuhusu upungufu wa wauguzi nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali
itaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo Wauguzi na
Wakunga na kuwapanga katika maeneo yenye upungufu zaidi.
Awali,
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Khamis Kigwangalla alisema baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali
wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua watumishi wa Sekta ya Afya
bila ya kufuata taratibu, jambo ambalo si sahihi.
Mkutano
huo umehudhuriwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Kigwangalla, Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania
Bw. Paul Magesa, Mbunge wa Lindi Mjini Bw. Hassan Kaunje, Mbunge wa
Kuteuliwa Mama Salma Kikwete(MB) Viti maalum.
Wengine
ni Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Gustav Moyo, Mwenyekiti wa Baraza
la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bw. Stewart Mbelwa.
Wengine
ni Mbunge wa Viti Maalumu, Hamida Abdallah, Mkurugenzi Msaidizi wa
Mafunzo ya Uuguzi Bw. Ndementria Vermund, Rais wa Chama cha Madaktari
Tanzania Dkt. Obadia Nyongole na wawakilishi wa wauguzi kutoka mikoa
yote nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 04, 2017.
0 comments:
Post a Comment