Tuesday, April 25, 2017

Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi kufufua upya mchakato wa Katiba mpya

Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi ameishauri Serikali kuleta Bungeni Sheria itayohuisha mchakato wa Katiba mpya ili kazi iliyobaki ya kupigwa kwa kura ya maoni  (Referendum ) iweze kupata uhalali wa kisheria. 

Chumi aliyasema hayo wakati wa mjadala wa Hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria Leo tarehe 25 Mei,  2017.

Akichangia mjadala huo, Chumi alisema kuwa, wakati wabunge wengi wakitaka Serikali kutenga bajeti  kwa ajili ya kura ya maoni, wanasahau kuwa sheria iliyoundwa kuongoza mchakato wa Katiba Mpya ilishamaliza Muda wake (expire).

'Mhe Mwenyekiti kazi kubwa na fedha nyingi zilitumika katika suala la Katiba mpya, kazi iliyobaki ni ndogo Sana, ni muhimu Sasa Serikali ikaanzisha mchakato wa kuleta sheria ili kuhuisha mchakato huo'.

Mbunge huyo wa Mafinga Mjini alisema kuwa, nchi nyingi zilizounda Katiba Mpya zilitumia Muda mrefu na mfano ni Kenya ambapo ilichukua zaidi ya miaka kumi ili kupata Katiba mpya, hivyo ili kukamilisha mchakato huo, ni vema sheria ikahuishwa kukamilisha jambo Hilo. 

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamaganda Kabudi alisema kuwa hoja hiyo ni ya msingi lakini ni vizuri kama Taifa tukajipa muda wa kutosha ili kukamilisha suala hilo kwa ufanisi.

'Wakati huu ambao bado kama vumbi halijatulia si vizuri Sana kufanya jambo hili kwa kuharakisha, cha muhimu dhamira ipo ' alimalizia Prof. Kabudi.

Mchakato wa Katiba mpya ambao uliundiwa Bunge Maalum la Katiba ulibakisha hatua moja muhimu ya kupiga kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Pendekezwa, suala ambalo litahitaji kuhuishwa kwa sheria ili kuupa mchakato huo uhalali wa kisheria.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More