Jafari Mwanyemba
***
MADIWANI wa Manispaa ya Dodoma wamemwondoa Meya wao, Jafari Mwanyemba
kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye kutokana na kumtuhumu
kuhusika na tuhuma mbalimbali zikiwamo za ubadhirifu wa fedha.
Kura hizo zilipigwa mjini hapa kwenye Mkutano Maalumu wa Madiwani wa kujadili tuhuma dhidi ya Meya Mwanyemba.
Kati ya madiwani wa manispaa hiyo 56, 47 ndio walipiga kura ya kutokuwa
na imani naye dhidi ya kura nne zilizodai kuwa na imani naye, wakati
kura moja iliharibika na madiwani wanane hawakupiga kura.
Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa, Godwin Kunambi
alisema kuanzia saa 8.30 adhuhuri hiyo, Mwanyemba si Meya wa Manispaa
ya Dodoma na kutokana na kanuni za manispaa, Naibu Meya Jumanne Ngede
ndiye atakayekuwa akiongoza hadi uchaguzi wa kuziba nafasi
utakapofanyika miezi miwili kuanzia sasa.
Alisema kutokana na kanuni za halmashauri hiyo namba 4 (8), baada ya
Tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa kurudisha ripoti kwa mkurugenzi katika
kipindi cha siku 14, alitakiwa kuwasilisha kwenye mkutano maalumu wa
madiwani kwa uamuzi wa tuhuma dhidi ya meya huyo ambapo madiwani
wameamua kumng’oa kwa kupigia kura.
Kutokana na kupigwa kura ya kumng’oa, kanuni za halmashauri zinamruhusu
aliyekuwa Meya wa Manispaa ndani ya mwezi mmoja kukata rufaa kwa Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
0 comments:
Post a Comment