NA MZIDALFA ZAID(ARUSHA)
MKUU wa wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara,Bi Sara Msafiri amepiga marufuku kwa mtu yeyote yule kufanya shughuli za kibiashara za mazao nje ya soko la Kimataifa la ENDAGAW na kwamba mtu atakayegundulika akiendelea kufanya biashara nje ya soko hilo hatua kali na za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Mkuu wa wilaya huyo ametoa agizo hilo kwenye uzinduzi wa Bodi ya soko hilo uliofanyika katika Mji wa Katesh na kuongeza kuwa uchunguzi wa muda mrefu umebaini kwamba idadi kubwa ya wafanyabiashara wamekuwa wakiwadhulumu wakulima kwa kununua mazao yao kwa bei ya chini kwa lengo la kukwepa ushuru wa serikali kwa kuyafuata mazao hayo kwa wakulima. Awali katika taarifa ya soko hilo iliyosomwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hanang,na Kaimu Afisa Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika,Minde Nanagi amefafanua kwamba soko hilo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na limeshaanza kutoa huduma kwa majaribio tangu msimu wa mazao mwaka jana. Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Mji wa Hanang,wameonyesha furaha yao kwa kuzinduliwa kwa Bodi ya soko hilo na kwamba kwa hivi sasa wamekuwa na uhakika wa kuuza mazao yao katika soko hilo la Kimataifa la Endagaw. Wameweka bayana wananchi hao kuwa awali kabla ya kuwepo kwa soko hilo wafanyabiashara waliokuwa wakinunua mazao wilayani humo walikuwa wakiwatapeli. Soko hilo la Kimataifa la Endagaw limejengwa kwa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika(A.D.B.) kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na lina uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 2,500 kwa mara moja zinazoweza kununuliwa na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kwa mkupuo,kinyume na ilivyo sasa ambapo wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifuata mazao kwenye mashamba ya wakulima na hivyo kuharibu bei ya mazao.
0 comments:
Post a Comment