Jeshi
la Polisi Mkoani Iringa linaendelea kumshikilia Mwenyekiti wa zamani wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa, Dk Jesca Msambatavangu anayetuhumiwa kumshambulia
na kumsababishia maumivu makali mwilini mwanamke mmoja, ambaye jina lake bado
halijafahamika.
Mpaka
jana jioni wakili wake aliyetajwa kwa jina moja la Chaula na wadhamini wake
walikuwa wakiendelea na taratibu za kumdhamini kada huyo wa CCM wa zamani huku
kukiwa hakunataarifa zozote zinazoashiria kupewa dhamana hiyo.
Akizungumza
kwa kifupi kuhusiana na tukio hilo juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,
Julius Mjengi alisema kada huyo wa zamani wa CCM alikamatwa juzi mchana,
akituhumiwa kutenda kosa hilo wiki iliyopita akiwa na wenzake ambao majina yao
yamehifadhiwa kwakuwa wanaendelea kutafutwa.
RPC
Mjengi alisema Msambatavangu na wenzake wanadaiwa kumshambulia mwanamke mmoja
mkazi wa Kibwabwa (hakutajwa jina kwasababu za kiupelelezi) na kisha kumchoma
sindano takoni ambayo mwanamke huyo hajui ni ya kitu gani.
Msambatavangu
alikuwa miongoni mwa vigogo wa CCM ‘waliotumbuliwa’ hivi karibuni na kufukuzwa
uanachama katika Mkutano Maalum wa CCM uliofanyika Machi, mwaka huu.
Baadhi
ya marafiki na ndugu wa jirani wa Dk Msambatavangu jana walikusanyika nje ya
ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa katika kile kilichoonekana kutaka
kujua hatma ya mwanasiasa huyo ambaye pia ni mfanyabishara maarufu mjini
Iringa.
Kabla
ya kutoa amri iliyowataka watu hao kutawanyika katika eneo hilo kwa kile
kilichoelezwa walikuwa katika mkusanyiko usio halali, Jeshi la Polisi
liliwazuia watu hao kuingia ndani ya uzio wa ofisi hiyo ya RPC.
Baadhi
ya waandishi wa habari waliofika katika ofisi hizo nao hawakupata fursa ya
kuingia ndani ya uzio wa ofisi hizo ili kukutana na RPC kwa lengo la kupataa
taarifa kamili ya kukamatwa kwa mwanasiasa huyo.
0 comments:
Post a Comment