Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva amewataka
wanasiasa walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu waache kujitangaza kuwa
walishinda, akisema wanapotosha wananchi.
Kauli
hiyo ya Jaji Lubuva imekuja siku chache baada ya aliyekuwa mgombea
urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa kudai kuwa kama si matokeo
kuchakachuliwa, alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu wananchi
walishaichoka CCM na wakawa wanataka mabadiliko.
Lowassa
alisema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari ofisini
kwake, akisema yeye na Ukawa walishinda kwa kishindo isipokuwa matokeo
yalivurugwa makusudi ili CCM iendelee kubaki madarakani.
Jana,
akiwa kwenye mkutano wa tathmini kati ya NEC na asasi za kiraia kuhusu
utoaji elimu kwa mpigakura uliofanyika Dodoma, Jaji Lubuva alisema
uchaguzi umeshapita na kilichobaki sasa ni kufanya kazi tu.
Bila
ya kutaja jina la mwanasiasa huyo, Jaji Lubuva alisema kama kuna mtu
alishindwa katika uchaguzi uliopita, ajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu
ujao mwaka 2020.
“Hata wananchi wanawashangaa kwa kuwa wao ndio walioamua ni nani anafaa kuwaongoza,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema
kuwa NEC ilikuwa inapokea matokeo ya uchaguzi kutoka majimboni na
kuyasoma kama yalivyotumwa na katika hilo hakuna wakala hata mmoja wa
chama ambaye aliyapinga matokeo hayo.
“Sasa
nashangaa kuna baadhi ya wagombea wanaotaka Tume ifukuzwe kazi eti tu
kwa sababu wao hawakushinda. Naomba ifahamike kwamba katika kila
uchaguzi duniani kuna kushinda na kushindwa.
"Sasa
kama kila atakayeshindwa atataka tume ifukuzwe kazi hapatakuwa na tume
ya uchaguzi kwa sababu kila atakayekuwa anashindwa atakuwa anataka tume
ifukuzwe kazi,” alisema Jaji Lubuva.
Chadema,
ambayo iliungana na vyama vitatu kuunda Ukawa, iliitaka NEC kusitisha
utangazaji matokeo ikidai kuwa kilichokuwa kikitangazwa ni tofauti na
takwimu walizokusanya kutoka majimboni. Lakini NEC ikaendelea kutangaza.
Baadaye,
Chadema ililalamika ikidai kituo chao cha kukusanya na kujumlisha
matokeo kilivamiwa na polisi na kompyuta kuchukuliwa na hivyo kuvuruga
ufuatiliaji wao wa matokeo.
Kwa
upande wake mkurugenzi wa huduma kutoka NEC, Emmanuel Kavishe alisema
kuwa Tume inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na Katiba na kwamba hata
siku moja haijawahi kumpendelea au kumuonea mtu yeyote.
Katika uchaguzi wa urais, John Magufuli alipata kura milioni 8.8 huku Lowassa akipata milioni 6.07.
0 comments:
Post a Comment