Friday, February 5, 2016

MADIWANI WA CHADEMA WALALAMIKA KUBURUZWA NA MSTAHILI MEYA WA JIJI LA MWANZA.

John Pambalu ambae ni diwani wa Kata ya Butimba (Chadema) akiwasilisha mchango wake katika kikao cha baraza la madiwani Jijini Mwanza.

Na:George Binagi-GB Pazzo
Madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Jijini Mwanza, wamemlalamikia Mstahiki Meya wa Jiji hilo kwa madai ya kuliongoza kibabe baraza la Madiwani.

Wakizungumza baada ya kikao cha baraza la Madiwani kilichoketi hii leo, Madiwani hao wamelalamikia kitendo cha kuzuiliwa kujadili taarifa ya Kamati ya fedha iliyowasilisha katika kikao hicho kwa madai kwamba jukumu la baraza hilo ni kupitisha taarifa hiyo na si kuijadili.

Samwel Range ambae ni diwani wa Kata ya Pamba pamoja na John Pambalu ambae ni diwani wa Kata ya Butimba (Wote Chadema), wamesema wamesikitishwa kuona kanuni za vikao zikivunjwa huku madiwani wakinyimwa fursa ya kujadili taarifa ya kamati ya fedha iliyowasilishwa.

“Tumeshuhudia utawala wa kibabe ukianza katika halmashauri yetu huku mhe.Mwenyekiti wa kikao (Meya) pamoja na Mkurugenzi wake wakiamua kutofuata kanuni na kuamua kufuata matakwa yao binafsi. Tumeletewa taarifa ya kamati ya fedha, wakati wa kujadili tunaambiwa hakuna sababu ya kuijadili isipokuwa kuipitia na kuiidhinisha taarifa hiyo, kitu ambacho madiwani wa Chadema na Upinzani tunakilalamikia”. Alisema Pambalu.

Nae Samwel Range amesema “Kamati ya fedha haina mamlaka ya kuidhinisha chochote ndani ya halmashauri ya Jiji la Mwanza. Inapaswa ilete taarifa yake na kuileta katika baraza la Madiwani ambapo sisi tunauwepo wa kuikubali au kuikataa”.

Hata hivyo malalamiko hayo yamepingwa na James Bwire ambae ndie Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza na diwani wa Kata ya Mahina (CCM), ambapo amefafanua kwamba malalamiko ya madiwani wa Chadema hayana msingi wowote ikizingatiwa kwamba taarifa iliyowasilishwa na kamati ya fedha iliishajadiliwa ndani ya kamati hivyo hakukuwa na umuhimu wa kuijadili tena ndani ya baraza la madiwani bali kuipokea na kuipitisha.

Baraza la Madiwani Jijini Mwanza linaundwa na Madiwani 24 na linaongozwa na Chama cha Mapinduzi CCM kwa upande wa Mstahiki Meya pamoja na Naibu Meya ambapo kuna Madiwani 19 kutoka CCM huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kikiwa na Madiwani Watano.


Kutokana na Uwiano huyo, Madiwani wa Chadema wanalalamika kuburuzwa katika baraza hilo kutokana na uchache wao, madai ambayo hata hivyo yanapingwa na Madiwani kutoka CCM ambao wanasema suala lolote lenye maslahi kwa umma linapewa nafasi sawa ndani ya baraza hilo bila kujadi itikadi za vyama vya siasa. 
Kushoto ni Naibu Meya Jiji la Mwanza, Katikati ni Mstahiki Meya na Kulia ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza
Waheshimiwa Madiwani Jijini Mwanza
Waheshimiwa Madiwani Jijini Mwanza
Watendaji wa Idara mbalimbali Jijini Mwanza.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More