Serikali mkoani Kilimanjaro imeuagiza uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya
Mlima Kilimanjaro (Kinapa), kuwachukulia hatua askari wanaodaiwa
kuwanyanyasa wanawake wanaoingia katika Misitu ya Nusu Maili kukata
nyasi na kuokota kuni.
Mkuu wa mkoa huo, Amos Makala alitoa
agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha
Mshiri wilayani hapa.
Alisema katika ziara aliyofanya kwenye
vijiji vinavyozunguka msitu huo, wanawake wamekuwa wakilalamika
kufanyiwa vitendo vya ukatili, ikiwamo ubakaji na kupigwa wanapokutwa na
askari hao wakikata nyasi kwa ajili kulisha ng’ombe na kuokota kuni za
kupikia.
“Kinapa najua wapo baadhi ya askari wenu ambao siyo
waaminifu, wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya kikatili na vya kinyama
wanawake wanaoingia katika Msitu wa Nusu Maili. Kwa hiyo nawaagiza
kuwachukulia hatua za kisheria mara moja,” alisema Makala Mkuu huyo wa
mkoa alisema vitendo hivyo ni vya aibu na vya kusikitisha kwa taasisi
kubwa ya umma.
“Mtu mzima hawezi kusimama kwenye hadhara ya watu
wengi namna hii na kusema uongo katika mambo makubwa kama kubakwa na
kutembezwa kwenye hifadhi siku nzima, kupigwa na kukalishwa kwenye
siafu,” alisema Makalla.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho,
Veronica Mlay alisema wamekuwa wakiingia katika hifadhi hiyo siku za
Jumatano na Jumamosi ambazo wameruhusiwa kukata nyasi na kuokota kuni,
lakini baadhi ya askari wa Kinapa wanapowakuta huwafanyia vitendo vya
unyanyasaji.
Kaimu mhifadhi wa hifadhi hiyo, Charles Ngendo
alisema vitendo hivyo viliwahi kulalamikiwa miaka ya nyuma katika ofisi
yake na kuvishughulikia.
0 comments:
Post a Comment