Meneja wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Mkoa wa Dar es Salaam,
Lawrence Mwalumwelo na wenzake wawili wamefikishwa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu kujibu mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka.
Mwendesha
Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sophia
Nyanda akishirikiana na Veronica Chimwanda mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,
Respicius Mwijage aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Ofisa Tawala,
Modester Fumbuka na Ofisa Manunuzi, Radecunda Massawe, wafanyakazi wa
TPC.
Chimwanda alidai kuwa kati ya Agosti Mosi na Oktoba 31,
2010 washtakiwa hao walitumia vibaya madaraka yao kwa kuipa mkataba wa
kutafuta vibarua kampuni ya Technical Merchantile Service bila kupata
kibali kutoka bodi ya zabuni.
Vilevile ilidaiwa kuwa Septemba 26
,2011 washtakiwa hao walitumia vibaya madaraka yao kwa kuiongezea
kampuni hiyo mkataba wa kutafuta vibarua kutoka Septemba 30 hadi Desemba
31, 2011 bila ya kuishirikisha bodi hiyo.
Ilidaiwa kuwa Januari
Mosi, 2012 washtakiwa hao waliiongezea tena kampuni hiyo mkataba wa
kutafuta vibarua kutoka Januari Mosi, 2012 hadi Machi 30, 2014 bila ya
kuishirikisha bodi hiyo. Washtakiwa hao walikana mashtaka.
Washtakiwa hao waliachiwa baada ya kutumiza masharti ya dhamana na kesi hiyo kuahirishwa hadi Machi 17.
0 comments:
Post a Comment