Thursday, February 11, 2016

Watanzania Wapelekwa Uganda Kupiga Kura

Mgombea wa urais katika uchaguzi ujao nchini Uganda, Amama Mbabazi amedaia kuwa kundi la raia wa kigeni wamekuwa wakisafirishwa hadi nchini humo kwa ajili ya kumpigia kura Rais Yoweri Museveni.

Mbabazi ambaye ni mgombea huru alisema, mamia ya raia kutoka nchi za Tanzania na Rwanda wamekuwa wakiwasili nchini humo ili kukisaidia chama tawala na mgombea wake kushinda kwenye uchaguzi huo.

Mwanasiasa huyo ambaye kabla hapo alikuwa waziri mkuu chini ya utawala wa Rais Museveni, alitahadharisha wananchi kuwa macho na mwenendo huo, huku akiwataka kuchukua hatua kuzuia aina yoyote ya udanganyifu.

Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari alisema yeye binafsi pamoja na timu yake ya kampeni itaendelea kuwa macho kufuatilia mwenendo huo.

“Watu wana njia nyingi za kufanya udanganyifu. Idadi kubwa ya Watanzania wamekuwa wakiwasili nchini kwa ajili ya kupiga kura. Pia, tumeshuhudia watu wakitoka Rwanda na kupiga kura.

"Tumebaini njama zao na sisi wananchi lazima tuwe macho kuwabaini watu hao siku ya kupiga kura itapowadia,”
alisema Mbabazi. Uchaguzi Mkuu nchini humo utafanyika Februari 18.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More