Saturday, February 13, 2016

DK. KINGWANGALLA ATOA SIKU 60 KWA HOSPITALI YA KANDA YA RUFAA MBEYA, KUNUNUA MASHINE YA CT-SCAN

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dk. Hamisi Kingwangalla amefanya ziara, Februari 12, 2016 katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Nyanda za juu kusini- Mbeya, na kutoa maagizo mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mashine CT-Scan ndani ya siku 60 huku akibainisha kuwa endapo watazembea basi watawachukulia hatua kali na kuwajibishwa watendaji na uongozi wa Hospitali hiyo.
 
Dk. Kigwangalla alifika hospitalini hapo majira ya saa tisa alasiri na kutembelea idara mbalimbali za hospitali hiyo kuona jinsi ya ufanyaji kazi ambapo ndipo alipobaini ukosefu wa mashine hiyo ya CT-Scan pamoja na vifaa vingine muhimu ambavyo alibainisha kuwa hata uongozi wa Hospitali hiyo walikuwa na uwezo wa kuvinunua bila kutegemea Serikali.

Baadhi ya idara ambazo, Dk. Kingwangalla alitembelea ni pamoja na kitengo cha kutolea huduma kwa wagonjwa (OPD), Kitengo cha upasuaji, wodi ya upasuaji, duka la dawa la hospitali hiyo, wodi ya wanawake, wodi ya wanaume, watoto na kitengo cha Maabara ambapo kisha alipata kuongea na wafanyakazi pamoja na uongozi mzima wa Hospitali.
Dk.Kigwangalla alitoa wasaha mwingi kusikiliza kero za wafanyakazi hao kuongea lile linalowakabili bila kuogopa ili aweze kujua matatizo na changamoto zinazowakabili.

"Hospitali kubwa kama hii hapa Mbeya na wataalam wote mlionao mnashindwa kufanya biashara!, Mnategemea tu Serikali? lini mtakuwa na CT-scan kwa upande wenu? wakati mnaingiza Milioni 500 kwa mwezi?" alihoji Dk. Kigwangalla.

Dk.Kigwangalla aliwaambia uongozi wa hospitali hiyo ina fursa na uwezo wa kufanya jambo kubwa kwani pia ina uwezo hata wa kukopa fedha kutoka mashirika ya bima ya afya.

Aidha, Dk Kigwangalla amewataka uongozi wa Hospitali hiyo kuwa wabunifu katika uendeshaji wao ikiwemo kutengeneza jengo la kisasa la matibabu ya kulipia, kujenga nyumba za wafanyakazi ambapo amewapa mikakati hiyo imeanza na pindi atakaporejea tena hospitali hiyo.

DSC_3499

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dk. Hamisi Kingwangalla akisisitiza suala la Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Nyanda za juu kusini- Mbeya kununua mashine ya CT-scan ndani ya siku 60, huku akiahidi kuwachukulia hatua kali ya kuwawajibisha watendaji watakaozembea katika hilo.

kigwangalambeya2

Baadhi ya wafanyakazi na madaktari wa hospitali hiyo wakifuatilia mkutano huo wakati Naibu Waziri Dk.Kigwangalla (hayupo pichani) wakati wa alipofanya ziara Februari 12,2016. Wafanyakazi hao waliweza kutoa maoni yao mbalimbali ikiwemo suala la motisha na uboreshaji wa mishahara pamoja na ukosefu wa vitendea kazi ikiwemo kitengo cha maabara.

kigwangala mbeya

Mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo ya rufaa Mbeya akiuliza akitoa maoni yake kwa Naibu Waziri Dk.Kigwangalla.

kigwazz

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali ya Kanda ya rufaa Mbeya, Thomas Isidori akitoa fursa kwa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla (kulia) kuzungumza na wafanyakazi katika mkutano wake huo.

kigwangala2

Naibu Waziri wa Afya, Dk.Kigwangalla akipita katika moja ya maeneo ya hospitali hiyo ya Kanda ya rufaa Mbeya sambamba na wenyeji wake...

kigwaz

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla akitazama moja ya kipimo cha mgonjwa ambacho hata hivyo ilieleza kuwa kilipimwa nje ya Hospitali hiyo na kuletwa hapo ambapo alipotaka kujua kwa nini imekuwa hivyo kwa hospitali kubwa kama hiyo alielezwa kuwa hawana mashine ya CT-Scan ndipo alipoutaka uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha mashine hiyo inapatikana ndani ya siku 60 kuanzia hiyo Februari 12.

kigwangala mbeya6

Naibu Waziri wa Afya, Dk.Kigwangalla akipata maelezo ya moja ya mashine ndani ya maabara ya hospitali hiyo ya Kanda ya rufaa Mbeya. Hata hivyo ameelezwa mashine hiyo ni ya zamani sana hivyo ufanisi wake ni mdogo huku wakimweleza kuwa inatakiwa wapatiwe mpya ilikuendana na kasi.

kigwangaz

Naibu Waziri wa Afya, Dk.Kigwangalla akimjulia hali Mtoto Edger Emmanuel (2) anayepatiwa matibabu ya mguu wake katika wodi hiyo ya watoto kitengo cha upasuaji.

kigwaz11

Naibu Waziri wa Afya, Dk.Kigwangalla na Kaimu Mkurugenzi, Thomas Isidori wakimjulia hali Mzee Lazaro Mwakapunga aliyelazwa hospitalini hapo.

kigwanga1

Naibu Waziri wa Afya, Dk.Kigwangalla akipatiwa maelezo namna ya mfuko wa malipo wa ki-elektroniki unaotumiwa hospitalini hapo na Kaimu Mkurugenzi, Thomas Isidori. Hospiatli hiyo inatumia mfumo huo ambapo imeweza kufanikiwa katika ukusanyaji wake wa mapato.

kigwangala

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla akipokelewa na Katibu wa Hospitali hiyo, Maryam Msalale wakati wa kuwasili katika ziara hiyo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More