Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kushika dola licha ya upinzani mkali
kutoka vyama vingine vya siasa hasa vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwake, yanaandika historia nyingine ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake Februari 5, 1977.
Chini
ya Baba wa Taifa Mwalimu, Julius Nyerere chama hicho ambacho ni cha
pili kwa ukubwa barani Afrika kikitanguliwa na ANC cha Afrika Kusini,
kinajivunia mambo mengi yaliyokifanya kudumu mpaka sasa wakati vyama
vikongwe vya nchi nyingine kama Zambia (UNIP), Kenya (Kanu) na Malawi
vikiwa vimeshaondolewa madarakani.
Nape ataja siri ya mafanikio
Katibu
wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye anasema mfumo wa chama
hicho kujiimarisha kimtandao kuanzia ngazi ya shina kwa maana ya balozi
wa nyumba kumi mpaka taifa umekifanya kiendelee kuwa kimbilio la
wananchi wengi hadi kufikia kupata wanachama zaidi ya milioni sita,
kutoka wanachama wachache waliokuwapo miaka iliyopita.
“Chama
chetu kimeendelea kuwa na sura ya kitaifa, kalenda inayojulikana ambayo
imekuwa ikiruhusu chaguzi kila baada ya miaka mitano na kuifanya
Tanzania kuwa nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia,” anasema.
Yapo baadhi ya mambo ambayo chama hicho kinajivunia kwa miaka 39 tangu kizaliwe.
Kuendelea kushika dola
Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Patrick Myovela anasema mafanikio ya
chama hicho ni pamoja na ushindi kwenye chaguzi mbalimbali
zilizowawezesha kuendelea kushika dola.
“Tumepata
ushindi uliotuwezesha kushika dola katika chaguzi kuu zilizofanyika
zaidi ya mara sita. Tumeishi kwenye shabaha ya chama chetu ile inayotaka
kuendelea kuwa madarakani, tukiunda na kusimamia Serikali,” anasema.
Myovela
ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, CCM bado
inaaminiwa na Watanzania wengi ndiyo maana wameendelea kukipa kura na
kukiwezesha kuunda Serikali. Hiyo imetokana na imani ya wananchi juu ya
chama hicho.
Nape
anasema mara zote CCM imekuwa ikichagua mgombea urais atakayeweza
kushika bendera ya chama hicho kwa umakini zaidi kwa kuzingatia matakwa
ya wananchi kwa wakati husika.
Uongozi wa kupokezana
Kati ya vitu ambavyo vimeiletea sifa kubwa Tanzania ni pamoja na kuwa na uongozi wa kupokezana madaraka.
Wakati
nchi nyingine ikiwamo Uganda, Burundi na Zimbabwe zikivurugana kutokana
na vyama vinavyotawala kushindwa kuenzi dhana ya kupokezana, tayari
Tanzania imeshapitia awamu tano za uongozi na kila awamu ikiongozwa na
rais tofauti.
“Baada
ya kuongoza miaka 23, Mwalimu Nyerere aliamua kung’atuka akimuachia
Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye aliingia kwa kupigiwa
kura licha ya kuwapo kwa mfumo wa chama kimoja,” anasema Nape.
Anasema
uongozi huo wa nchi kupokezana ulimfanya Rais wa Awamu ya Tatu
Benjamin Mkapa kushikilia usukani akimpokea Mwinyi hadi mwaka 2005
alipomkabidhi Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na mwaka jana Rais
John Magufuli.
Myovela anasema ni dhahiri taswira nzuri ya uongozi wa nchi inatokana na uimara wa chama kilichopo madarakani.
Demokrasia ya vyama vingi
Licha
ya kuwapo kwa mabadiliko ya kidemokrasia hususan mfumo wa vyama vingi
ulioasisiwa na CCM yenyewe mwaka 1992, chama hicho kimeendelea kushamiri
huku kikishinda chaguzi zote kuu na zile za mitaa.
Nape anasema wakati CCM iliamua kuasisi mfumo huo, wananchi wengi walitamani kiendelee kuwa peke yake.
“Kumbuka
kwamba wakati wa kura ya maoni ya kuendelea kuwa na mfumo wa chama
kimoja au kuwa na vyama vingi vya siasa, Watanzania wengi walipendekeza
kuendelea kuwapo kwa chama kimoja, lakini kutokana na demokrasia, CCM
iliamua kuruhusu mfumo wa vyama vingi kuanza nchini,” anasema.
Mpaka
sasa Tanzania ina vyama vya siasa zaidi ya 20 vilivyosajiliwa, vingi
vikiwa vimefanikiwa kushiriki katika chaguzi mbalimbali.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Iringa, Enock Ugulumu ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa anasema kama kingeendelea kuwa na mgombea
mmoja kila kinapoingia madarakani, uhakika wa kuwapo mpaka leo
usingekuwapo.
“Mfumo
wa kubadilishana uongozi ndiyo siri kubwa ya ushindi wa CCM,
hatung’ang’anii madaraka kwa sababu Katiba ya CCM imeruhusu demokrasia
tangu ndani, mpaka nje kwenye umma.
"Vinginevyo Mwenyekiti wa CCM Taifa asingetaka kutoka kwa miaka yote, angebaki kuwa yuleyule,” anasema.
Vipo vyama ambavyo vimeshindwa kuzingatia mfumo wa kubadilishana madaraka kwa kuwa na viongozi wale wale tangu kuanzishwa kwake.
Katiba Mpya
Mchakato
wa upatikanaji wa Katiba Mpya unaonyesha namna ambavyo CCM
ilivyofanikiwa kupokea na kufanyia kazi ushauri na mapendekezo
yanayotolewa na wananchi kutoka katika kada zote.
Nape
anasema CCM inajivunia kuwa na mchakato huo hata kama haujafikia
mwisho. Anasema uwepo wa rasimu iliyopita kwenye Bunge la Katiba
kunaifanya CCM ionekane inasikiliza maoni ya Watanzania na kuyatumia
inapowezekana.
“Ni chama kilichodumu kwa muda mrefu, kinajivunia kuwa kisikivu na kutimiza mahitaji ya Watanzania.” Anasema bila nia njema ya kukubali mchakato huo uwepo, usingeanzishwa na kufikia hatua ya kura za maoni ilipo sasa.
Kulinda na kudumisha amani nchini
Nape anasema katika tunu za taifa mbazo CCM inajivunia kuziendeleza tangu uhuru kuwa ni kulinda na kudumisha amani.
Katika
miaka yote, CCM imekuwa ikiagiza na kusimamia kuhakikisha Serikali
inalinda na kudumisha misingi imara ya amani iliyoasisiwa na waanzilishi
wa taifa.
Hata
hivyo, anasema CCM imeshiriki katika harakati za kutafuta ukombozi wa
nchi majirani ili kujihakikishia usalama ndani na nje ya nchi
Uhuru, umoja na mshikamano .
Myovela
anasema ni ukweli usiopingika kuwa umoja na mshikamano uliopo nchini
unatokana na usimamizi mzuri wa Serikali inayoundwa na chama hicho.
Anasema
kutokuwa na ubaguzi wa aina yoyote ile ikiwamo udini, ukabila, rangi
wala ukanda unatokana na misingi mizuri iliyowekwa na chama hicho tangu
kuundwa kwake.
Nape
anasema kitendo cha kuwa na ilani za uchaguzi zinazogusa maisha ya watu
wa kila kada, kimeisaidia Serikali kutimiza wajibu wake.
“Kila
mwaka wa uchaguzi, CCM imekuwa ikiisimamia Serikali katika kutimiza
majukumu yake kupitia ilani ya uchaguzi. Ukisoma ilani zote utagundua
CCM haikurupuki, inafanya mambo yake kwa umakini mkubwa. Hili
tunajivunia,” anasema Nape.
Anasema
msingi wa utawala bora lazima uendane na kile ambacho chama kingependa
wananchi wake wafanyiwe kwa kuiagiza Serikali kupitia ilani yake.
Anasema
viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa taarifa ya utekelezaji wao wa
majukumu kwa chama ili kipate nafasi ya kukosoa na kusonga mbele.
Utawala bora
Nape anasema Watanzania wameshuhudia uanzishwaji wa mikoa, wilaya, kata na vijiji vipya ili kuwasogezea huduma karibu.
Maazimio
Anasema
kuna maazimio mbalimbali likiwamo Azimio la Mtowisa lililotaka kila
kaya kujitosheleza kwa chakula na Azimio la Zanzibar lililofungua
Demokrasia ya ndani ya CCM, haya yote yamechangia katika mafanikio ya
CCM.
0 comments:
Post a Comment