MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) ameungana na watanzania wengine kumpongeza Rais Dk John Magufuli kwa sera yake ya kutumbua majipu huku akiahidi kumtajia wafanyabiashara wakubwa wa mjini Iringa aliosema ni wanaokwepa kodi.
Akiwashukuru wapiga kura wa mjini hapa
kwa kumchagua kwa mara nyingine tena kuwa mbunge wao na kuwachagua madiwani 14 kutoka
Chadema kati ya madiwani 18 wanaounda halmashauri ya manispaa ya Iringa katika
mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Mwembetogwa, mjini hapa
Mchungaji Msigwa alisema:
“Katika kutumbua majipu tunamuunga mkono
Dk Magufuli na niahidi tutamwonesha wafanyabiashara wakubwa wanaokwenda kodi.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na wabunge
wa viti maalumu wa chama hicho, Suzan
Mgonakulima na Grace Tendega, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe na
madiwani wote wa chama hicho, Mchungaji Msigwa alisema mbali na wafanyabiashara
hao, baraza lao madiwani litahakiki taarifa za ulipaji kodi, hasa za majengo,
zinazokihusu Chama cha Mapinduzi (CCM) mjini Iringa.
“Yapo madai yanayoonesha CCM hapa Iringa
hailipi kodi za majengo yake mbalimbali. Majengo hayo ni pamoja na uwanja wa
Samora, jengo la CCM Mkoa, vibanda vya biashara maarufu kama vibanda vya
kitimoto na vingine vya maduka ya pombe, ofisi na uwanja wa sabasaba,” alisema.
Alisema watafanya uhakiki katika majengo
hayo yote ili kujilidhisha kama ule uhalali wa serikali yao unaowawezesha
kukusanya kodi kutoka kwa watu wengine, unatumika pia kukusanya kodi katika
miradi yao mbalimbali inayotakiwa kulipiwa kodi.
Alisema ili waweze kufikia malengo ya
kimaendeleo waliyojiwekea katika kipindi cha miaka mitano ijayo, baraza lao la
madiwani limepanga kusimamia kwa nguvu zake zote ukusanyaji wa kodi kwa
kuhakikisha wenye kingi wanalipa zaidi ya wale wenye kidogo.
Akizungumzia migogoro ya ardhi mjini
Iringa, mbunge huyo alisema chanze chake ni ukosefu wa ardhi na akashauri wale
wenye mashamba ndani ya manispaa wafanye utaratibu wa kuyakabidhi manispaa na
walipwe fidia ili mashamba yao yapimwe viwanja vitakavyogaiwa kwa wananchi.
Akizungumzia mikakati ya halmashauri
yake, Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe alisema halmashauri yake imepanga
kuongeza makusanyo yake ya mwaka kutoka Sh Bilioni 2.5 za sasa hadi Sh Bilioni
7 katika kipindi cha 2016/2017.
Alisema halmashauri hiyo itahakikisha inakusanya kodi zake zote kikamilifu na sehemu ya fedha zitakazopatikana zitatumika kununua gari la kubeba wagonjwa na kubeba taka ili kuboresha huduma katika sekta ya afya na usafi wa mazingira.
0 comments:
Post a Comment