Thursday, January 28, 2016

Watuhumiwa 7 wa Makontena Waliokuwa Wametoroka Wakamatwa

Wafanyakazi saba kati ya wanane wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) waliotuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,019 na magari 2,019 kutoka bandarini ambao walitoroka, wamepatikana na tayari wanaendelea kuhojiwa na polisi juu ya tuhuma hizo.
Watumishi hao ni kati ya watuhumiwa 15 wa TPA waliotangazwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuwa wameshiriki kuondosha makontena na magari hayo kutoka katika bandari kavu saba bila kulipa ushuru wa Bandari.

Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi alisema jana kuwa mfanyakazi mmoja kati ya hao wanane, hajapatikana; na anaendelea kusakwa na polisi ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.

“Wote walishapatikana kasoro mtumishi mmoja, Happygod Naftali, ambaye huyu alishaacha kazi siku nyingi baada ya viongozi kuanza kufuatilia suala hilo; lakini bado polisi wanaendelea kumsaka,” alisema Ruzangi.

Mkuu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alithibitisha watuhumiwa hao, kukamatwa na kwamba bado wanaendelea kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo.

“Ni kwamba tunaendelea na upelelezi wetu,” alisema Sirro licha ya kuwa hakutaka kutaja idadi ya wafanyakazi wa TPA ambao wamepatikana. “Kwa kweli idadi nitaitoa siku nitakapozungumza na waandishi wa habari wiki hii,” alifafanua.

Watumishi waliokuwa wanasakwa na polisi waliopatikana kwa mujibu wa Ruzangi ni Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Bonasweet Kimaina, Zainab Bwijo na Nathan Edward.

Watumishi hao wanaungana na watumishi wengine saba John Elisante, Leticia Masaro, Christina Temu, Merina Chawala, Adnan Ally, Masoud Seleman na Benadeta Sangawe waliokamatwa na kuhojiwa kuhusu sakata hilo. Watumishi hao saba, kwa mujibu wa Sirro, tayari walishapelekwa mahakamani.

“Ukiacha wale saba ambao tumeshawafikisha mahakamani, hawa wengine bado tuko nao tunaendelea kufanya upelelezi,” alieleza.

Wafanyakazi hao wanatuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,884 na magari 2,019 ambayo yalitoroshwa kutoka katika Bandari Kavu (ICD) saba bila kulipiwa ushuru wa bandari na hivyo kuipotezea Serikali mapato ya Sh bilioni 48.55.

Kuhusu mawakala 280 waliopewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo yao makao makuu ya TPA namna ya walivyohusika kulipia makontena hayo, Ruzangi alisema mamlaka yake inajipanga kutoa taarifa kamili juu ya suala hilo.

“Tunaendelea kuandaa taarifa ya kilichotokea na kilichobainika kuhusu mawakala hao, tutatoa taarifa hivi karibuni,” alisema Meneja Mawasiliano huyo.

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, uongozi wake umeibua ufisadi wa kutisha ambao ulikuwa unafanywa Bandari ya Dar es Salaama kwa kuwashirikisha wafanyakazi wa TPA na mawakala pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Kwa mara ya kwanza upotevu wa makontena 349 uligundulika baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutinga bandarini na kubaini makontena hayo kutolewa bandari kavu bila kulipiwa kodi. 

Upotevu huo ulifanya vigogo wa TRA, akiwemo Kamishna Mkuu Rished Bade na makamishna wengine kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani.

Baadaye Majaliwa alibaini upotevu wa makontena 2,431 yaliyoondolewa bandari kavu bila kulipiwa ushuru wa Bandari.

Katika sakata hilo, baadhi ya mawakala wa forodha walifungiwa kufanya biashara na TPA Sakata la mwisho ni la kupotea kwa makontena 11,019 na magari 2,019, ambayo yaliondolewa kwenye ICD saba bila kulipiwa ushuru wa bandari na kuipotezea serikali mapato ya Sh bilioni 48.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More