SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema imejipanga kuhakikisha Uchaguzi
Mkuu wa marudio utakaofanyika Machi 20, mwaka huu unakuwa huru na haki
kwa kupambana na makundi ya aina ya watu mbalimbali wanaokusudia kufanya
fujo ikiwemo kuwazuia wenye sifa wasipige kura.
Hayo
yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed
Aboud wakati alipozungumza na watendaji wa Serikali wakiwemo wakuu wa
wilaya na mikoa na baadhi ya vikosi vya ulinzi mjini Chake Chake, Pemba.
Alisema
zipo taarifa kwamba kipo kikundi cha watu kimeandaliwa kwa ajili ya
kufanya vurugu katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu, ikiwemo kuwazuia watu
washindwe kwenda kupiga kura kwa malengo ya kisiasa zaidi.
Aboud
alisema, Serikali haiwezi kuvumilia watu wa aina hiyo pamoja na vitendo
hivyo ambavyo vinakwenda kinyume cha demokrasia ya mfumo wa vyama vingi
inayotoa fursa zaidi kwa watu kushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwa
kuwachagua viongozi wanaowataka.
“Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti kuhakikisha kwamba wananchi wote
wenye sifa ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa marudio wanatimiza
azma ya kidemokrasia ya kupiga kura na vitendo vya kihuni vyenye lengo
la kusababisha fujo na vurugu kamwe havina nafasi,” alisema Aboud.
Alifafanua
zaidi kuwa chama ambacho hakipo tayari kushiriki katika Uchaguzi Mkuu
wa marudio hakina sababu ya kuanza kuweka mikakati ambayo itasababisha
watu wengine kushindwa kutekeleza malengo ya kidemokrasia ya kuchagua
viongozi wanaotawaka kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Alisema,
vipo viashiria vya vitendo vya vurugu na fujo vimeanza kujitokeza hivi
sasa kwa baadhi ya watu kuandika vikaratasi vyenye muelekeo wa kuleta
uchochezi wa kisiasa pamoja na mtizamo wa kuwagawa wananchi wa visiwa
viwili vya Unguja na Pemba.
Aboud
alisema msimamo wa serikali tayari umetangazwa kupitia Tume ya Uchaguzi
ya kufanya uchaguzi wa marudio Machi 20, baada ya ule wa Oktoba 25,
mwaka jana kufutwa baada ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali.
Alisema
ni wajibu wa vyama vyote vilivyoshiriki katika uchaguzi wa Oktoba 25
kushiriki tena katika mchakato huo ambao ndio halali utakaowafanya
wananchi kupata viongozi wao kwa njia ya kidemokrasia ya uchaguzi.
“Msimamo
wa Serikali ya Mapinduzi upo wazi kwamba vyama vya siasa vilivyoshiriki
katika Uchaguzi Mkuu uliofutwa wa Oktoba mwaka jana vinapaswa kujiandaa
na uchaguzi wa marudio,” alisema.
0 comments:
Post a Comment