Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewataka wananchi hususani madereva, makondakta na abiria wanaosafiri kutoka kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani kuwafichua waalifu wanaoingiza silaha ndogondogo, madawa ya kulevya, na wahamiaji haramu kupitia usafiri wa mabasi hayo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Naibu
Kamishna wa Polisi SIMON SIRRO ameyasema hayo leo alfajiri alipokuwa
akizungumza na madereva, makondakta na abiria na kusema kuwa wahaalifu wengi
wanatumia usafiri huo katika kutekeleza uhalifu wao bila kugundulika, na kuwataka
wananchi kutoa taarifa zitakazo saidia kuwafichua waalifu hao.
Kuhusu suala la uingizaji wa silaha katika jiji la Dar es
Salaam Kamanda SIRRO amesema silaha hizo zinaingizwa na wahaalifu kupitia
usafiri wa mabasi toka nchi jirani zenye migogoro ya kisiasa na vita kama
Burundi, Congo DRC na Somalia kupitia nchi ya Kenya ambapo zote kwa pamoja
zinapakana na Tanzania.
Akizungumzia madawa ya kulevya alisema kuna changamoto kubwa
ya kudhibiti biashara hiyo harama inayoleta madhara makubwa kwa jamii yetu. Amesema
madawa ya kulevya mengi yanaingizwa nchini kupitia baharini na maziwa makuu
kisha yanasafirishwa kwa usafiri wa mabasi kutoka mikoa ya pembezoni. Amewaomba
wanachi kuwafichua wahalifu hao kwa kutoa taarifa polisi pindi wanapomtilia
shaka mtu yeyote.
Amewaasa watanzania kuacha utamaduni wa kuaminiana kupita
kiasi na watu wasiowafahamu na kuwataka kutopokea vitu vidogo vidogo kama juice
au maji ambvyo huchanganywa na madawa ya kulevya na kusababishwa kuibiwa au
madhara mengine.
Aliwataka wananchi washirikiane na Jeshi la Polisi kwa kutoa
taarifa kupitia namba 0754 280 994
wakati wote ili kupata huduma stahiki.
SIMON SIRRO – DCP
KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
0 comments:
Post a Comment