OFISA
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) mkoani Dodoma,
Emmanuel Meta (37) ameuawa kufuatia kupigwa na kukatwa mapanga cha watu
ambao mpaka sasa hawajafahamika.
Hata hivyo Jeshi la Polisi linamshikilia mtu mmoja kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu majira ya saa 6:15 usiku katika eneo la Area C manispaa ya Dodoma.
Kwa
mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi wa
Polisi (ACP), David Mnyambuga, Ofisa huyo wa PCCB alifariki dunia wakati
anapatiwa matibabu baada ya kupigwa na watu ambao hakuwafahamu.
Alisema
mtoa taarifa wa awali wa tukio hilo, Athuman Mtengwa ambaye pia ni
mfanyakazi PCCB, mkazi wa Area “D” alieleza kuwa, Januari 20, saa 6:15
usiku akiwa nyumbani kwake alipigiwa simu na Emmanuel (marehemu) ambaye
ni mfanyakazi mwenzake pia ni rafiki yake wa karibu.
Alisema
Meta alimweleza kuwa anaomba msaada wa kupelekwa hospitali kutibiwa kwa
kuwa amepigwa na watu wasiofahamika wakati akirudi nyumbani kwake
akitokea baa ya Rose Garden iliyopo Area “C” jirani na nyumbani kwake
kwa matembezi.
Baada
ya Mtengwa kufika alipiga honi ndipo Meta alitoka nje na kufunga mlango
na geti kwa kufuli na kuingia katika gari kuelekea Hospitali ya Mkoa wa
Dodoma na wakiwa njiani hali yake ilibadilika na kukosa nguvu na
kushindwa kujimudu kwa lolote.
Alisema wakati akiendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alifariki dunia.
Kaimu
Kamanda alisema uchunguzi wa mwili wa marehemu umefanyika ambapo
amekutwa na jeraha kichwani linalovuja damu, alitokwa na damu puani na
masikioni, uvimbe katika jicho la kulia na michubuko midogo mikononi.
“Mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea,” alisema Kaimu Kamanda.
Alitoa
wito kwa mtu au watu wenye taarifa kuhusiana na tukio hili washirikiane
na Jeshi la Polisi kuwafichua watu waliofanya uhalifu huo ili sheria
ichukue mkondo wake.
0 comments:
Post a Comment