MKURUGENZI
wa Mashitaka (DPP) ameamua kukata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya kesi ya
uchochezi inayomkabili mwanaharakati wa Kiislamu Shehe Ponda Issa Ponda.
Mwanasheria
Mwandamizi katika ofisi ya DPP, Bernard Kongola amesema kuwa Serikali
inapinga kuachiwa kwa Shehe Ponda ambaye alishitakiwa kwa makosa ya
uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
“Tayari
tumeomba tupatiwe nakala ya hukumu pamoja na nyaraka za mwenendo wa
shauri hilo ili upande wa mashitaka tuweze kuandaa rufaa yetu Mahakama
Kuu,” alisema.
Kwa
mujibu wa mwanasheria huyo, tangu waombe kupatiwa nakala ya hukumu hiyo
katika mahakama hiyo ya hakimu mkazi, hakimu ambaye alikuwa anasikiliza
kesi hiyo bado hajawapatia upande wa mashitaka hukumu ambayo imechapwa.
“Hatujui
kuna tatizo gani, maana tunapoomba kupatiwa nakala ya hukumu, hakimu
amekuwa anatuambia kwamba bado hawajamaliza kuichapa, kwa kweli hii
inashangaza,” alisema.
Novemba
30 mwaka uliopita, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Morogoro, Mary Moyo
alimwachia huru Shehe Ponda kwa maelezo kuwa upande wa mashitaka
ulishindwa kuthibitisha pasi shaka yoyote mashitaka dhidi ya
mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Wakati
kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa, upande wa mashitaka uliita mashahidi
wanane kwa lengo la kuthibitisha makosa dhidi ya Shehe Ponda ambaye
alikuwa anatetewa na Mawakili wa kujitegemea Juma Nassoro na Abubakar
Salum.
Shehe
Ponda alifikishwa katika mahakama hiyo Agosti 19, 2013 akikabiliwa na
mashitaka matatu likiwemo la kukaidi amri ya Mahakama ya Kisutu
iliyomtaka awe mhubiri amani katika jamii likiwa ni sharti la kifungo
cha mwaka mmoja nje baada ya kumtia hatiani katika kesi ya jinai.
Upande
wa mashitaka ulidai kuwa Shehe Ponda alitenda kosa Agosti 10, 2013
katika eneo la Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege iliyoko katika Manispaa
ya Morogoro.
Ilidaiwa
kuwa siku hiyo kiongozi huyo wa kidini alidaiwa kutoa maneno ya
uchochezi ya kuhamasisha jamii kinyume na maelekezo ya mahakama.
Katika
mkutano huo Shehe Ponda anadaiwa kusema maneno haya, “Ndugu Waislamu
msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwani
kamati hizo zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na
kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati
za ulinzi na usalama za msikiti, fungeni milango na madirisha ya
misikiti yenu na muwapige sana.”
Kauli
hiyo inadaiwa kwenda kinyume cha amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya
Kisutu, Dar es Salaam, iliyotolewa mahakamani hapo na Hakimu Victoria
Nongwa, Mei 9, 2013 ambayo ilimtaka ndani ya mwaka mmoja kuhubiri amani
na asifanye jambo lolote la uvunjifu wa amani na badala yake ahubiri
suala la amani, ambayo ni kinyume cha Kifungu cha Sheria Namba 124 cha
Mwaka 2002.
Shitaka
la pili lililokuwa likimkabili Shehe Ponda ni uvunjifu wa sheria
Kifungu cha 129 cha Makosa ya Jinai kuwa siku hiyo, alitoa maneno ya
uchochezi yaliyohatarisha kuathiri imani za watu wengine.
Katika
hati ya shitaka hilo, ilinukuu kauli ya Ponda kuwa “Serikali ilipeleka
Jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa
kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi
wake ni Waislamu. Lakini Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa
Loliondo walipokataa Mwarabu asipewe kipande cha ardhi ya uwindaji baada
ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni
Wakristo.”
Shitaka
la tatu anadaiwa kutenda kosa kinyume cha sheria kifungu cha 390 na 35
kwa kuchochea maneno dhidi ya wananchi wakati wa kongamano lililofanyika
Agosti 10, 2013 Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.
0 comments:
Post a Comment