Watu
watatu wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Mchukwi wilayani hapa Mkoa
wa Pwani, wamekufa baada ya kupigwa na radi jikoni wakati mvua
zikinyesha.
Tukio
hilo limetokea jana jioni katika kijiji hicho. Inadaiwa kuwa radi hiyo
ilianza kupiga mti uliokuwa pembezoni mwa jiko hilo kabla ya kuwaua
ndugu hao.
Shuhuda
wa tukio hilo, Amina Tenge ambaye pia ni Ofisa Mtendaji wa kijiji
hicho, alisema waliwachukua ndugu hao na kuwapeleka Hospitali ya Misheni
ya Mchukwi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya majeraha waliyopata.
“Tulipofika hospitali walikuwa wameshafariki tayari,” alisema Tenge.
Mganga
wa zamu wa Hospital hiyo, Esther Mtini aliwataja marehemu hao kuwa ni
Desteria Simba (40), Deborah Simba (2) na Amani Matimbwa (6).
Alisema baada ya kuifanyia uchunguzi miili hiyo, walibaini kuwa Desteria alikuwa ameungua kifuani, tumboni na shavuni.
“Amani aliungua tumboni na katika sehemu zake za siri na Deborah hakuwa na jeraha lolote,” alisema Dk Mtini.
Akizungumzia
ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu aliwataka wananchi
kuepuka kukaa chini ya miti au karibu na miti katika kipindi hiki
ambacho mvua zinaendelea kunyesha kwani ni hatari kwa maisha yao.
“Mvua
hizi zinazoendelea kunyesha sasa zina madhara kwa sababu zinaambatana
na radi na upepo mkali, lazima tuchukue tahadhari kwa kuacha kukaa chini
ya miti au jirani ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea,” alisema Babu.
0 comments:
Post a Comment