Baadhi ya mitambo iliyotelekezwa kwenye Kiwanda cha kutengenezea Zana za Kilimo ZZK |
Mitambo ambayo ilikuwa ikitumika kutengenezea Zana za Kilimo katika kiwanda cha ZZK Iyunga jijini Mbeya ikiwa imetelekezwa |
Niranjan Bandi, aliyejitambulisha kuwa ndiye Mkurugenzi mkuu wa shughuli zinazoendelea katika kiwanda cha ZZK chini ya kampuni ya CMG akiwapa maelezo waandishi wa habari. |
Waandishi wakitoka katika kiwanda cha ZZK huku wakijiuliza maswali mbali mbali kutokana na walichokikuta ndani ya kiwanda hicho |
Baadhi ya waandishi wakichungulia ndani ya majengo ya kilichokuwa kiwanda cha kutengeneza sabuni HISOAP Kushuhudia kama kuna kilichosalia. |
Huu ndiyo muonekano wa ndani ya majengo ya kilichokuwa kiwanda cha kutengenezea sabuni HISOAP kukiwa hakuna kitu licha ya kuwepo Mlinzi |
Muonekano wa Jengo la kiwanda cha HISOAP lililotelekezwa ili hali serikali ya awamu ya tano ikisisitiza kuwa serikali ya Viwanda |
CHAMA Cha Waandishi wa
Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania(TAJATI) katika kutekeleza majukumu yake
kimefanya ziara katika viwanda vine vilivyopo Iyunga jijini Mbeya na kushuhudia
baadhi vikiwa vimetelekezwa.
Waandishi hao 15 kutoka vyombo mbali mbali ambao ni
wanachama wa TAJATI, walifanya ziara hiyo iliyoanzia katika majengo
yaliyokuwa ya Kiwanda cha kutengenezea sabuni kilichokuwa kikijulikana kwa jina
la HISOAP kilichopo Iyunga jijini Mbeya na kukutana na majengo hayo yakiwa
yametelekezwa.
Mbali na kutelekezwa kwa
majengo hayo,pamoja na kuwepo kwa mlinzi
ambaye alikiri kulinda majengo ambayo ndani yake hajui kilichomo kwa kupitia
matundu ya mlangoni,wanahabari hao walishuhudia ndani kukiwa hakuna hata mtambo
mmoja ulichosalia na na matanki makubwa yanayoendelea kuoza nje.
“Mimi nalinda hapa kwa
maagizo ya bosi wangu lakini huko ndani hakuna shughulli yoyote inayofanyika
kwani hata hizo mboga zilizolimwa ni mali ya walinzi wenzetu ndiyo wamelima,sijui
humo ndani kama kuna mitambo sijawahi kuona milango ikifunguliwa hata mwenye
funguo simjui” alisema Mlinzi ambaye alitaka jina lake lihifadhiwe kwa usalama
wake.
Aidha katika ziara hiyo
timu ya waandishi ilifika katika majengo ya kilichokuwa kiwanda cha serikali,
Kiwanda cha kutengenezea zana za kilimo maarufu kwa jina la ZZK ambapo timu
hiyo ilipokelewa na raia mmoja wa kigeni mwenye asili ya kiasia, Niranjan Bandi, aliyejitambulisha kuwa ndiye
Mkurugenzi mkuu wa shughuli zinazoendelea hapo chini ya kampuni ya CMG.
Katika maelezo yake kwa
waandishi wa habari Bandi alisema ndani ya kiwanda hicho kuna shughuli za
kutengeneza vipuri vya magari, uunganishaji wa matrekta madogo ya kilimo(powertiller
) kutoka China na kwamba zana za kilimo wameshindwa kutengeneza kutokana
uchakavu wa mitambo iliyopo na imepitwa na teknolojia.
Aliongeza kuwa ifikapo
januari 15 mwaka huu wanatarajia kuanza kutengeneza mabati baada ya kupata
mtambo kutoka China ambao hivi sasa unafanyiwa marekebisho kabla ya kuanza kazi
sambamba na uanzishwaji wa kiwanda cha kuzalisha bia cha Serengeti.
Wakati mwekezaji huyo
akijieleza na kuonyesha mashaka makubwa ya uzalishaji kuwa ni changa la macho,Waandishi
wa habari walishuhudia mitambo iliyokuwa
ya kutengenezea zana za kilimo ikiwa imetekelezwa bila kufanya kazi ndani ya
majengo hayo ambapo Mkurugenzi huyo alisema hawana uwezo wa kuiendesha.
Baada ya kukamilisha
mahojiano na Mkurugenzi huyo waandishi hao walielekea moja kwa moja katika
kiwanda cha Malumalu cha Marmo Granito ambapo walitembelea mitambo ya kuchonga na
kukata mawe na bidhaa mbali mbali zinazotokana na miamba ya asili.
Mkurugenzi wa Marmo,Salim
Jessa alisema tangu walipoanza uwekezaji katika Mkoa wa Mbeya wameanza kupata
masoko nje ya nchi ikiwemo India,Italia na kutafuta masoko mengine nchini China ambako watakuwa wakiuza malighafi
zilizoongezwa thamani kwa ajili ya matumizi mengine.
Alisema changamoto kubwa
ni ushindani wa soko baada ya kampuni zingine kujitokeza na kuanza kutengeneza
bidhaa zinazotokana na mawe ya asili kama wao sambamba na uingizaji wa bidhaa
zilizochakachuliwa kutoka nje kwa lengo la kuharibu soko.
Ziara hiyo ya TAJATI
ilihitimishwa katika kiwanda cha Bia cha TBL ambapo waandishi walitembezwa
kiwandani hapo na kisha kupata muda wa kuuliza maswali kutoka kwa wahusika.
Akizungumza na wanachama
hao, Meneja wa Kiwanda cha Bia Mbeya, Waziri Jemedari alisema licha ya
mafanikio waliyoyapata katika uzalishaji wanakabiliwa na changamoto kubwa
ambazo ni miundombinu mibovu, gharama kubwa za maji na umeme sambamba na
mlundikano wa vinywaji kutoka nje ya nchi vinavyoharibu bei ya vinywaji
vinavyozalishwa nchini.
Jemedari alisema bia
nyingi zinaingizwa nchini kutoka nje zinauzwa bei ya chini hivyo kupelekea
wateja wengi kukimbilia na kuua soko la vinywaji vya ndani.
Na Mbeya yetu
0 comments:
Post a Comment