SHIRIKA
la Viwango Tanzania (TBS), limeamuru shehena ya mafuta ya petroli
iliyoagizwa kutoka Falme za Kiarabu irejeshwe ilikotoka kutokana na
kubaini hayana ubora unaotakiwa kwa matumizi ya magari na mitambo.
Akitoa
taarifa hiyo Dar es Salam jana, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Joseph
Masikitiko alisema, vipimo vya maabara vya sampuli ya mafuta hayo
vimeonesha kuwa hayafai kwa matumizi.
Alisema
hayo ni matokeo ya ukaguzi wa hivi karibuni wa shehena hiyo yenye ujazo
wa tani za metriki 38,521.018 katika meli ya MT. Ridgebury John B,
yaliyokuwa yasambazwe na kuuzwa nchini.
Alisema, "Vipimo
vinaonesha kuwa baadhi ya matakwa ya viwango vya mafuta ya petroli
hayajafikiwa, hivyo kuamuru yarejeshwe yalikotoka. Kiwango cha ubora cha
mafuta ya petroli ni TZS 672:2012/ EAS 158:2012 ambacho hakikufikiwa".
Matakwa
ya kiwango ambacho mafuta hayo hayakukidhi ni pamoja na kuwa na
kemikali zilizo na oksijeni ndani yake ambazo husababisha madhara kwenye
injini za magari na mitambo.
Alisema,
"Kiwango cha petroli hakiruhusu uwepo wa kemikali hizo kwenye mafuta
hayo kwa sababu zinaua injini, kuhatarisha afya za watu na kuharibu
mazingira kutokana na kusababisha moshi mchafu mwingi".
Alifafanua
kuwa mafuta hayo yameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuvuta maji au
mvuke na kuwa sehemu ya petroli, kiasi cha kuifanya iwe na maji mengi
ambayo ni hatari kwa injini za magari na mitambo.
Pia,
alieleza uhafifu mwingine katika mafuta hayo kuwa ni kupungua kwa nguvu
ya kuendesha injini au mitambo hivyo kusababisha uharibifu na hasara.
Aliongeza
kuwa, mvuke unapokuwa mwingi kwenye petroli husababisha mtiririko wa
mafuta kwenda kwenye injini kutokuwa mzuri, huku kemikali aina ya
benzene iliyoonekana kuzidi katika petroli hiyo ikiwa ni chanzo cha
kansa kwa wanaotoa huduma ya uuzaji wa mafuta hayo.
Sambamba
na hayo, Masikitiko aliongeza kuwa walibaini kuwa uhafifu katika mafuta
hayo unaongeza wingi wa ujazo wa nishati hiyo pasipokuwa na uhalisia na
kisha kutoa nguvu isiyolingana na wingi wake. Alisema, madhara yake ni
mnunuzi kulipia wingi wa mafuta usio na thamani halisi.
Aliwahakikishia
watumiaji wa mafuta kuwa, shirika hilo litahakikisha linafanya ukaguzi
katika meli zote zenye mafuta yanayokusudiwa kusambazwa nchini ili
kuzuia yasiyo na ubora yasiingizwe sokoni.
Katika
hatua nyingine, Tbs ilisema kuwa iliagiza vilainishi vya mitambo na
magari vya kampuni ya HASS Petroleum (T) Limited vyenye ujazo wa lita
16,080 kutoka Falme za Kiarabu virejeshwe vilikotoka pia kwa sababu ya
kukosa ubora unaofaa kwa matumizi na kwamba mwagizaji alitekeleza agizo
hilo tangu Desemba 31 mwaka jana.
Ewura yazungumza
Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imekiri kufahamu kuhusu suala
hilo na kueleza wananchi kuwa licha ya mafuta hayo kutakiwa kurejeshwa
yalipotoka, bado nchi ina akiba ya petroli inayoweza kutumika hadi
shehena nyingine iletwe.
"Wananchi
wasiwe na wasiwasi," alisema Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Ewura,
Titus Kaguo. Alisema kwa siku nchi inatumia lita za petroli 2,700,000,
na kwamba kila metriki tani moja ya petroli huwa na lita 700,000.
"Kwa
maana hiyo, lita 33,000,000 za petroli zilizokuja na kukataliwa endapo
zingeshushwa na kutumika nchini zingeweza kutosheleza mahitaji kwa zaidi
ya siku saba," alisema Kaguo .
Hata
hivyo, aliongeza kuwa si mafuta yote yanayoingia na meli bandarini
hushushwa kwa ajili ya matumizi ya nchi, bali mengine huwa safarini
kwenda nchi nyingine.
0 comments:
Post a Comment