Tuesday, January 12, 2016

TANESCO Watakiwa Kufanya Kazi na Wazalishaji Wadogo

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ameanza ziara yake Mkoa wa Njombe kwa kutembelea Mradi wa Kufua Umeme kwa kutumia mabaki ya miti ya Miwati (TANWAT.)
Baada ya kukagua mradi huo, Prof Muhongo ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufanya majadiliano na TANWAT ili waongeze uzalishaji kutoka Megawati 2.5 za umeme hadi kufikia Megawati 10.

Aidha, ameagiza TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini REA kufanya majadiliano na TANWAT ili kuanza kununua nguzo zinazozalishwa na kampuni hiyo yenye uwezo wa kuzalisha nguzo 120,000 kwa mwaka badala ya kununua nguzo hizo katika nchi za Kenya, Zambia, Uganda na Afrika Kusini.

"REA na TANESCO watakuja hapa kuangalia hizi nguzo na kufanya ukaguzi kama zinakidhi viwango vya TANESCO. Ikiwa zinakidhi viwango REA wawaelekeze Wakandarasi kununua nguzo za TANWAT kwa kufuata taratibu za manunuzi," ameongeza Prof. Muhongo.

Pia Prof. Muhongo amewataka TANESCO kubadilika kiutendaji na kuongeza wigo wa uzalishaji umeme kwa kuwatumia wazalishaji wakubwa, wa kati na wadogo ambao wote kwa pamoja watasaidia kuondoa tatizo la uhaba wa nishati hiyo.

Akikagua Mradi wa kufua umeme wa Uwemba, Prof Muhongo ameiagiza  TANESCO Njombe kuandaa orodha ya vyanzo vya umeme vinavyotokana  na maji vilivyo katika gridi na visivyo katika gridi na kujadiliana na wazalishaji  ili kukubaliana nao kuuziana umeme

"Uzalishaji umeme kutumia maji ndio rahisi zaidi. TANESCO angalieni orodha hiyo, wawaeleze Mikataba yao muone namna ya kuuziana umeme. Bila umeme huwezi kuzalisha ajira na bila umeme wa uhakika hatuwezi kuwa na viwanda vya kutosha," alisema.

Waziri Muhongo ameongeza kuwa ni wajibu wa Serikali kuwasaidia na kufanya kazi na wazalishaji wadogo wa umeme ili waweze kuongeza  kiwango cha uzalishaji umeme hivyo pia ameutaka Mkoa wa Njombe kufuatilia kwa pamoja na TANESCO suala hilo na kulifanyia kazi.

Vilevile, aliwataka TANESCO kukaa na wazalishaji wadogo ili kuangalia bei zao, jambo ambalo litaiwezesha Serikali kujua bei kwa lengo la kuhakikisha kwamba bei hizo hazimuumizi mwananchi.

Aidha, Profesa Muhongo aliwaagiza TANESCO kufanya ukarabati wa mashine zilizoharibika ili ziendelee kufanya kazi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Jackson Saitab aliahidi kuyafanyia kazi maagizo yote ya Waziri na kuongeza kuwa, nishati ni sekta muhimu hata katika uongezaji thamani ya mazao.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More