==>Makala hii inapatika kwenye ukurasa wa Facebook wa Zitto Kabwe
MTUMISHI wa Mungu afumaniwe kwa uzinzi na mke wa mtu, kesho asubuhi aamkie madhabahuni kuhubiri neno kisha waumini wapokee. Huko ni kumtania Mungu.
Mimbari ni kwa ajili ya wasafi. Ukiwa mchafu hufai kuhubiri neno. Maneno ya Mungu hayashereheshwi na mwenye uchafu. Maana mtu mchafu ni mtenda dhambi.
Mwandishi wa Habari na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, anataka kuhubiri neno. Waumini tunakataa. Maana asiye msafi hafai kuaminika kwa maneno yake.
Mhubiri neno hatakiwi kuwa ndumilakuwili. Hapaswi kuwa kigeugeu wala mshadadia uongo. Anatakiwa awe mkweli na siku zote aweze kuuishi ukweli wake.
Kubenea hana aibu kama Sepp Blatter, yule aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Kwamba pamoja na vielelezo vyote vya uharamia wake bado aling’ang’ania yeye ni msafi na akataka kuendelea kuongoza shirikisho hilo.
Kubenea ana roho ngumu kama Michel Platini, yule alikuwa Rais wa Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa). Kwamba pamoja na kila ushahidi kudhihirisha umafia wake wa kimtandao kwenye soka, bado alisimama imara kudai anaonewa.
Mwisho kabisa, Blatter na Platini, wamefungiwa na Kamati ya Maadili ya Fifa, kujihusisha na shughuli zote za soka kwa kipindi cha miaka nane.
Kubenea ni mwanaproganda asiyeuonea aibu uongo wake. Ni kama Muhammad Saeed al-Sahhaf, yule aliyekuwa waziri habari wa Iraq, wakati wa utawala wa hayati Saddam Hussein. Al-Sahhaf ndiye aliweka rekodi ya kuwa msema uongo bora mwaka 2003.
Wakati Marekani ilipoivamia Iraq mwaka 2003, Al-Sahhaf alikuwa na kazi ya kusema tu uongo kuwatisha Wamarekani. Tangu walipoanza mpaka walipouteka mji wa Baghdad, hakuna popote ambapo maneno ya Al-Sahhaf yalikuwa kweli.
Kubenea yupo vitani na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe. Anamshambulia mfululizo. Amejaliwa kumiliki magazeti, basi kwa vile mwenzake hana, ndiyo kila siku anaye tu!
Unaweza kutafuta mahali ambako Zitto na Kubenea waliwahi kugombana, huwezi kupaona. Zaidi, zipo taarifa kuwa Zitto amewahi kuwa msaada kwa Kubenea katika kazi zake.
Kwa nini kila siku Kubenea juu ya Zitto? Huwa anamtafuta nini? Kama kungekuwa na utofauti wa kijinsia kati yao, pengine ipo hoja ingezungumzwa. Ila kwa nidhamu kabisa lipo swali; Ya nini kila siku mwanaume juu ya mwanaume mwenzako? Unamfuatafuata wa nini? Kipi unakitafuta?
Upo msululu wa makala za Kubenea dhidi ya Zitto. Kwa Kubenea, Zitto hajawahi kuwa na jema kwake tangu mwaka 2009. Ni ajabu kuwa katika kipindi chote hicho Zitto hajawahi kujishughulisha kumjibu.
Hiyo inatoa picha moja kubwa kwamba Kubenea ni mwathirika wa maisha ya Zitto. Maana kuchukia kila kitu cha mtu ni ugonjwa. Kwani chochote atakachokifanya kitakupa majeraha.
Hata mwandishi mashuhuri, Marty Rubin aliwahi kusema: “To hate everything is to be wounded by everything.”
Kiswahili: Kuchukia kila kitu ni kujeruhiwa na kila kitu.
Tangu mwaka 2009, vipo vipindi vingi vya ushindi kwa Zitto. Katika maisha yake kisiasa jukwaani, jimboni na bungeni. Fikiria Kubenea ameumia kiasi gani katika kipindi chote hicho ambacho Zitto amekuwa akifanya vizuri.
Katika Uchaguzi Mkuu 2015, Kubenea aliandika makala kuwa Zitto hatashinda ubunge, matokeo yake asiyempenda alishinda. Hayo ni maumivu kiasi gani kwake?
Zitto alishinda na kurejea bungeni mwaka 2010, akashinda uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (Poac). Kubenea aliandika kuwa Zitto alisaidiwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete. Aliumizwa na ushindi huo!
Mwaka 2012 Zitto alionesha utaalam wake wa siasa za ndani ya bunge, pale wabunge walipopaza sauti kutaka mawaziri nane wang’oke kutokana na ufisadi, vilevile kushindwa kwao kusimamia ofisi walizokabidhiwa.
Zitto akasimama, akasema wabunge wanahangaika kwa sababu hawana mamlaka ya kuwajibisha mawaziri. Ila yupo mmoja ambaye akishughulikiwa, wengine wote watawajibika. Akamtaja huyo kuwa ni waziri mkuu.
Akaanza kukusanya saini za wabunge, kutimiza 70 ili awasilishe hoja ya kumng’oa waziri mkuu. Zitto alifanikiwa kushawishi wabunge wa vyama vyote bungeni ambao walisaini. Saini zikatimia. Rais Kikwete naye akawang’oa mawaziri waliokuwa wanatakiwa kuwajibishwa na kumuokoa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kwa kuchukua mantiki ya maneno ya Rubin, hili nalo lilikuwa shoka la kichwa kwa Kubenea kutoka kwa Zitto. Maana mafanikio ya Zitto ni pigo kwake. Anaumizwa na chuki zake. Chuki zikizidi ni ugonjwa usiotibika.
Mwaka 2012 Poac ilivunjwa na Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda. Kubenea akafurahia kwa sababu Zitto alipoteza uenyekiti wa kamati bungeni.
Makinda akaiunganisha Poac na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto akashinda uenyekiti wake, kwa mara nyingine Kubenea alinuna; “kwa nini kila siku Zitto haporomoki?”
Kuelekea mwishoni mwa mwaka 2014, Zitto aliiongoza PAC kwa mafanikio, kuiwajibisha serikali kutokana na wizi mkubwa uliofanyika Benki Kuu kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Zilikuwa fedha za mgogoro kati ya Tanesco na mwekezaji, Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL). Zikachotwa bila utaratibu. Watu waliiba.
Chini ya uongozi wa Zitto, PAC iliwezesha kuwajibika kwa aliyekuwa Mwansheria Mkuu, Fredrick Werema, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.
Kubenea aliumizwa na Zitto kutajwa kama shujaa wa kashfa ya Tegeta Escrow. Akasema Zitto hakufanya lolote kwa sababu kazi kubwa ilifanywa na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.
Kubenea anaumia sana mpaka namhurumia. Siwezi kumshauri kumpenda Zitto ila kwa ajili ya usalama wa afya yake, namshauri ajifunze kupenda vitu vizuri vinavyofanywa na watu asiowapenda.
Unaweza kuchukia watu lakini ukawa mpenda matokeo mazuri. Kwa hiyo hutaumia sana, kwani upande mmoja utachukizwa na mafanikio ya usiompenda, vilevile utachekelea matokeo bora. Kubenea ajifunze hili!
Sasa hivi Kubenea ndiyo kachangamka, kila siku makala zenye mrengo hasi dhidi ya Zitto. Inaelezwa ni mpango wa kuuendea uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC). Mimi sijui, ila ninachoona ni chuki.
Pengine Zitto hajibu kwa kutimiza maneno ya mhubiri wa Kanisa Katoliki, aliyeishi Roma Karne ya 13, Mtakatifu Thomas Aquinas aliyesema: “The principal act of courage is to endure and withstand dangers doggedly rather than to attack them.”
Kiswahili: Kitendo kikuu cha ujasiri ni kuvumilia na kuhimili hatari kwa ukimya bila kubweka kama mbwa kuliko kushambulia.
Hata hivyo, kitu cha kujiuliza ni hiki; Hivi Kubenea baada ya yote yaliyotokea, bado anataka aaminike kama mtu mkweli? Je, bado anataka kutuaminisha yeye ni mwandishi mzuri wa kuaminika anayesimamia misingi?
Je, hata baada ya kutuonesha sura zake nyingi za ufanyaji kazi? Hapana kabisa, haiwezekani!
Je, hata baada ya kuonesha kuwa yeye ni mwandishi maslahi? Miaka nane alimshambulia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuwa ni fisadi, mchafu, asiyesafishika hata kwa dodoki.
Kisha 2015, akageuka kumpigia debe Lowassa kuwa siyo fisadi na kwamba amekuwa akionewa tu. Huyuhuyu anataka tuamini kuwa yeye ndiye mkweli, anaowashambulia ndiyo wabaya.
Kwa nini kutokana na undumilakuwili wake tusiamini yeye ndiye mnafiki na maneno yake ndiyo uongo wake unapokuwa kazini?
Ukiwa muongo huwezi kumpenda mtu mkweli. Utamchukia kwa sababu uongo na ukweli hauwezi kufungamana. Kwa mantiki hiyo ni rahisi kutambua kuwa Zitto ni msafi kwa sababu anayemshambulia ni mchafu.
Mwandishi mashuhuri wa vitabu, raia wa Uingereza, William Makepeace Thackeray, aliyeishi kwa mafanikio ya uandishi wake Karne ya 19, alisema: “An evil person is like a dirty window, it never let the light shine through.”
Kiswahili: Mtu muovu ni sawa na dirisha chafu, haliwezi kamwe kupitisha mwanga mng’aavu.
Kwa kuchambua mapito ya Kubenea, bila shaka yoyote hayupo tena kwenye misingi ya kitaaluma ya uandishi wa habari. Anachwa nje na muongozo wa somo la Usawa wa Uandishi wa Habari (Journalistic Objectivity).
Katika Journalistic Objectivity, yapo mambo manne yanayozingatiwa. Mosi; Fairness (Haki). Pili; Disinterestedness (Kutokuwa na maslahi). Tatu; Factuality (Ukweli unaothibitishika). Nne; Nonpartisanship (Kutokuwa na upande).
Kubenea ni Chadema, kwa hiyo hayupo kwenye msingi. Hakatazwi kutoa maoni lakini hapaswi kujitambulisha kama mwandishi wa habari aliye mstari wa mbele kikazi kwa sababu hawezi kutenda haki. Anao upande tayari.
Na ndiyo maana vyombo vingi vya habari viliripoti kuhusu Mwenyekiti wa Chadema, Freema Mbowe, kufanya hamisho la mabilioni ya fedha nje ya nchi katika mazingira yenye kuashiria ama ufisadi au utakatishaji wa fedha haramu (money laundering) lakini hakuna gazeti lililo kwenye miliki ya Kubenea liliwahi kuripoti.
Zitto haelewani na Chadema, maana walimfukuza. Kubenea anapomshambulia anakuwa anakosea misingi kwa sababu yeye anao upande, kwa hiyo hawezi kumtendea haki Zitto.
Kampuni inayochapisha Gazeti la Mwanahalisi, Hali Halisi Publication, mbali na Kubenea, mkurugenzi wake mwingine ni Anthony Komu, huyu ni Mkurugenzi wa Fedha wa Chadema, yaani kwa lugha rahisi ndiye mweka hazina wa chama hicho.
Komu ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na alikuwa kwenye kikao siku kamati hiyo ilipowashughulikia Zitto, swahiba wake, Prof. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo.
Kutokana na hali hiyo, ni rahisi kushangaa Zitto akiandikwa vizuri na magazeti yaliyo chini ya miliki ya Kubenea na Komu kuliko kushambuliwa na kuchafuliwa.
Ajaze ukweli anavyoweza lakini pointi mbili kati ya nne ambazo nimezitaja kama mbeleko ya somo la Journalistic Objectivity, yaani Disinterestedness (Kutokuwa na maslahi) na Nonpartisanship (Kutokuwa na upande), zinamuondoa kwenye mstari.
Na hili linalosemwa kwamba naye anautaka uenyekiti wa PAC, sasa anamuona Zitto ni kikwazo, ndiyo anapoteza sifa kabisa.
Ni dhambi kubwa katika uandishi wa habari kuingiza vita binafsi (personal war) katika masuala ya kitaaluma.
Hata kama ingekuwa anachokiandika ni ukweli, huo ukweli unamuona Zitto upande wa ubaya tu? Na je, tangu mwaka 2009 Zitto alipochukua fomu ya kugombea uenyekiti Chadema, kushindana na Mbowe hajawahi kuwa na jema lolote la kuandikwa? Maana tangu hapo aligeuka msemwa vibaya wa Kubenea.
Kubenea akumbuke kuwa zilishapita nyakati aliaminika, baadaye ikagundulika ni kigeugeu. Ni vigumu kurudia makosa kwa kumwamini tena. Kiingereza kinanena: “It is a shame to fall twice over the same stump.” Kiswahili kinajibu: “Ni aibu kujikwaa kisiki mara mbili.” Aibu hii nani anaitaka kwa mara nyingine?
Kubenea siyo mtu wa misingi, vita binafsi huihamishia kwenye taaluma; Alikwaruzana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, moja kwa moja akaenda kumshughulia gazetini.
Ikawekwa picha, ikimuonesha Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete akifungwa kamba za viatu na mtu fulani ambaye haonekani vizuri. Picha ikaandikwa kuwa Makonda ndiye alikuwa anamfunga kamba Ridhiwani, ikaandikwa ukuu wa wilaya unatafutiwa mbali.
Tafsiri pale ni kuwa Makonda alimfunga kamba za viatu Ridhiwani ili ateuliwe kuwa mkuu wa wilaya na baba yake, Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.
Baadaye Ridhiwani alijitokeza na kufafanua kuwa aliyemfunga kamba za viatu hakuwa Makonda bali Deogratius Kessy ambaye ni mfanyakazi katika duka la mavazi la Sheria Ngowi, siku alipofuata mavazi yake.
Kwamba kwa kutaka kutimiza kiu yake ya kumshughulikia mtu, amekuwa tayari mpaka kupindisha ukweli, Kessy akaitwa Makonda!
Hoja hiyo inakamilisha pointi nyingine mbili kutoka kwenye Journalist Objectivity, Fairness (Haki) na Factuality (Ukweli unaothibitisha). Hajatenda haki, vilevile alichokiandika siyo ukweli unaothibitishika, kwani ni uongo.
Baadaye unakuja kugundua kuwa ndani ya Kubenea kuna tatizo la chuki. Na mtu anayesumbuliwa na tatizo hilo ni maradhi ambayo kitaalamu yanaitwa borderline disorder au kwa kirefu ni borderline personality disorder.
Borderline Disorder ni tawi katika mkusanyiko wa maradhi ya saikolojia yanayopatikana ndani ya somo linaloitwa Psychopathology.
Psychopathology; neno hili lina asili ya muunganiko wa maneno ya Kigiriki, psyche (nafsi), pathos (ugonjwa) na ology (somo). Maana ya moja kwa moja ya Psychopathology ni asili ya matatizo ya kisaikolojia, jinsi yanavyokua na dalili zake.
Yapo makundi nane ndani ya Psychopathology ambayo ni Major Depressive Disorder (kukosa mudi, kutokuwa na nguvu au kutamani kujiua nk), Bipolar Disorder (kuwa na mizuka mingi), Dysthymia (kukosa mudi) na Schizophrenia (kupingana na uhalisia, kuwa na mitazamo hasi na kuzungumza bila mpangilio)
Lipo Borderline Personality Disorder (rahisi kugombana na watu, kuwa na hisia kigeugeu, hasira nyingi na chuki), Pyromania (kuwa na shauku ya kupitiliza, kupenda vitu vya hatari, kufurahia majanga ya wengine), Phobias (kuwa na mapokeo yasiyo ya kawaida, kutohofia hatari na Bulimia Nervosa (tatizo la ulaji, kulakula hovyo na kujitapisha).
Katika makundi hayo nane ndani ya Psychopathology, yapo ambayo hayamhusu kabisa Kubenea lakini yapo haya manne;
1. SCHIZOPHRENIA
Schizophrenia ambayo tafsiri yake imebainishwa hapo juu, ikiwa ni kupingana na uhalisia, kuwa na mitazamo hasi na kuzungumza bila mpangilio.
Mtazamo hasi huendana na wivu. Hii ni sababu ya mashambulizi dhidi ya Zitto, vilevile kwa wengine kama ambavyo sasa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibroad Slaa, anavyotoneshwa na kalamu shambulizi ya Kubenea, wakati mwanzoni alikuwa msifiwa mkuu.
2. BORDERLINE DISORDER
Kwa dalili zilizomo ndani ya kundi hili, kwamba wahusika ni wale wapenda kugombana na watu, kuwa na hisia kigeugeu, vilevile hasira nyingi.
Kundi hili ndilo ambalo nilianza nalo na ndilo hasa limenifanya angalau niangalie kwa ufupi Psychopathology na matawi yake.
3. PYROMANIA
Hizi sifa za kuwa na shauku ya kupitiliza, kupenda vitu vya hatari, kufurahia majanga ya wengine zinamhusu mno Kubenea. Alishangilia mno Kafulila alipoitwa sisimizi na kutimuliwa Chadema, akachekelea pia Kitila, Mwigamba na Zitto walipofukuzwa na chama hicho.
Hili linaweza kubishiwa na mtu? Mara ngapi amejikuta akiingia kwenye migogoro na serikali kisha kuvuna huruma ya wananchi?
4. PHOBIAS
Tafsiri yake ipo juu lakini katika kipengele cha kukuza mambo inaeleweka. Tukio dogo la mtu asiyependwa na Kubenea linaweza kufanywa mjadala wa kujaza gazeti zima.
USHAURI
Aache chuki, na siyo kila wagomvi wa Chadema awaandame, vilevile haipendezi kuwa lazima awakumbatie watu pendwa na chama hicho.
Kugeuka na kumtetea Lowassa kwa sababu alibadilika na kuwa mtu pendwa wa Chadema ilimuondolea heshima na kumtupa nje ya maadili ya uandishi wa habari.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Cuf, Prof. Ibrahim Lipumba alipokuwa na utofauti na Chadema, alimkoma Kubenea. Na alipomkataa Lowassa kujiunga na Ukawa, akamkoma tena.
Yupo pia mwanasiasa mkongwe, Hamad Rashid Mohamed, aliyepata kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzania Bungeni, yeye kuna siku alimwambia Kubenea: “Tulia, kazi yenyewe tumekufundisha wenyewe.”
Ushauri wa juu ambao naweza kumpa Kubenea ni kwamba atenganishe maisha yake binafsi, ya kisiasa na taaluma. Akifanya hivyo atakuwa mwandishi mzuri.
Mwandishi mzuri hashambulii watu, ananyoosha ukweli kwa vipimo vyake. Palipo na zuri sifia, kwenye kasoro kosoa, siyo kushambulia mwanzo mwisho.
Mwisho nampongeza kwa ushindi wake mzuri alioupata kwenye kilele cha Uchaguzi Mkuu 2015, Jimbo la Ubungo. Akiwa mkweli kwenye utumishi wake atafanikiwa.
By Luqman Maloto
+255 713 355 71
0 comments:
Post a Comment