Monday, October 2, 2017

CRDB IWASAIDIE VIJANA WAWEZE KUTUMIA FURSA ZILIZOPO; WASIONE FAHARI KUJIITA ‘MABOMU’.

 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akikata keki kama ishara ya kuzindua wiki ya huduma kwa mteja katika benki ya CRDB, Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo na anayefuata ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba kabla hajamlisha keki wakati wa uzinduzi wa wiki ya huduma kwa Mteja katika benki ya CRDB.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ameishauri Benki ya CRDB Mkoa wa Singida kuwasiadia vijana elimu na mikopo ya kutambua na kutumia fursa zilizopo ili waachane na kauli za kujiita ‘mabomu yanayosubiri kulipuka’.

Dkt Nchimbi ametoa ushauri huo mapema leo wakati akizindua wiki ya huduma kwa mteja katika benki ya CRDB tawi la Singida huku akisisitiza benki hiyo kuwa bega kwa bega na Vijana.

“Vijana wetu wasione fahari kabisa kujiita mabomu yanayosubiri kulipa, Singida tuna fursa nyingi wasibweteke watumie benki hizi na nyinyi pamoja na benki nyingine jitahidini kuwashika vijana hawa wakipewa elimu ya ujasiriamali na mikopo wataifikisha Singida mbali kiuchumi”, amesema Dkt Nchimbi.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Singida umejipanga kuzalisha chakula cha kutosha ili uweze kulisha makao makuu ya nchi yaani Dodoma hivyo vijana wabadilike na wawe mabomba ya kusafirishia chakula na bidhaa mbali mbali.

Dkt Nchimbi ameongeza kuwa huduma za kibenki zinawasaidia watumishi wa umma katika kupanga matumizi ya pesa kwakuwa isingekuwa mishahara kupitia benki kungekuwa hakuna kinachosalia katika mishahara yao huku hicho kidogo kinachosalia kinakuwa cha muhimu sana.

Ameongeza kuwa kuelekea uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda huduma bora za kibenki ni hakikisho la safari hiyo kuwa salama na yenyewe uhakika huku benki zikiwa ni  mahali panapo waunganishawajasiriamali wakubwa kwa wadogo.

Ameongeza kuwa benki ya Crdb inaaminika ndio maana wajasiriamali na watumishi wengi wamekuwa wakiitumia hivyo na wateja wao pia wajenge tabia ya kuaminika hasa kwa kurejesha mikopo yao bila usumbufu.

“Watu wengi wamekuwa wakikopa bila ya kuwa na malengo hivyo kuishia lawama au hukopa kwa mazoea bila ya kujiandaa nini atafanyia huo mkopo, mteja wa hivyo anaweza kubadilika na kutokuwa mwaminifu hivyo benki mna jukumu kubwa la kutoa elimu ya kutosha wateja wenu”, amefafanua Dkt Nchimbi.

Ameeleza kua benki iendelee kuwaelimisha wajasiriamali na wananchi wengine kuwa kukopa sio aibu na mtu ambaye anakopesheka hiyo ni heshima hivyo atambue fursa hiyo na kuitumia vizuri.

Kwa upande wake Meneja wa Benki ya CRDB Singida Innocent Arbogast ameeleza kuwa benki hiyo inatoa mikopo kuanzia kwa wajasiriamali wadogo mpaka wakubwa pamoja na kutoa elimu pamoja na huduma za Sim banking, malkia akaunti na akaunti za watoto.

Arbogast amesema kuwa wiki ya huduma kwa mteja wataitumia vizuri kwa kuwatembelea wajasiriamali wote mitaani na kuelezea huduma zao kwakuwa wiki ya huduma kwa mteja ina lenga kuongeza uaminifu kati ya benki na wateja wao.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba amesema benki hiyo imekuwa ikiwasaidia watumishi ili waweze kutimiza malengo yao huku watumishi wakiwa waaminifu katika kurejesha mikopo hiyo.

ACP Magiligimba ametoa mfano wake yeye ambaye ameweza kujenga nyumba kutokana na mkopo wa benki hiyo hivyo watumishi wengine wasione aibu kukopa ila wawe wamejiwekea malengo mazuri ya matumizi ya mikopo hiyo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More