Friday, June 24, 2016

KAMPUNI YA TOMONI FARMS LIMITED YAFUNGUA DUKA NA MGAHAWA WA KISASA WA MAZAO YA KILIMO DAR

DSC_8003 


Mkurugenzi wa uendeshaji wa Kampuni ya Tomoni Farms Limited, Bwana Franklin Bagalla akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani wakati wa utambulisho wa tukio hilo mapema leo Juni 23.2016, Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Bwana Willybroad Alphonce.


Kampuni ya Tomoni Farms Limited, inayomilikiwa na wazawa, wakijishughulisha na Kilimo cha umwagiliaji cha mazao ya Matunda na Mbogamboga, wamefungua duka na Mgahawa wa Kisasa kwa ajili ya uuzaji wa mazao yao katika hali ya usafi na usalama wa hali ya juu uliopo eneo la jirani na Victoria, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari mapema leo Jijini Dar Es Salaam, wakati wa utambulisho wa duka hilo na shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo ya Tomoni Farms Limited, Mkurugenzi wa uendeshaji wa Kampuni hiyo Bwana Franklin Bagalla ameeleza kuwa, wameamua kuwasogezea watanzania bidhaa bora za kilimo ambazo watazipata moja kwa moja kupitia duka lao hilo na watajiona kama wapo shambani ama bustanini kwa namna ya uwekezaji wao walivyoweza kuuandaa ikiwemo mazingira safi na utunzaji wa kisasa kutoka shambani hadi kumfikia mlaji.

“Baada ya kuwekeza kwa miaka mine katika kilimo cha Matunda na Mboga mboga kwa kutumia teknolojia ya umwagiliaji, huku tukiwa na uhakika wa kutoa mazao Mwaka mzima, sasa tumewekeza katika miundo mbinu ya kuhakikisha mazao yetu yanawafikia walaji yakiwa katika hali ya usafi na usalama. Hivyo kupitia katika duka letu hili la kisasa hapa Dar es Salaam linatoa fursa kwa wananchi kujipatia bidhaa za kila aina na watazipata kwa hali ile ile kama zipo shambani na tunawakaribisha sana” alieleza Bwana Bagalla.

Aliongeza kuwa, Mazao yote yanavunwa na kusafirishwa katika magari maalumu kutegemea na uhitaji wa mazao hayo, na hupokelewa, kuchambuliwa na hatimaye kuhifadhiwa katika jokofu kubwa la baridi kuhakikisha kwamba ubora wa bidhaa unabakia kama ule wa shambani na baada ya hapo bidhaa hizo huuzwa kupitia duka hilo la kisasa na zingine hutumika katika mgahawa wao ambao pia unatengeneza aina mbali mbali za Juice nzito na nyepesi ambazo mara nyingi wataalam wa Afya wanashauri watu kutumia.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo ya Tomoni Farms Limited, Bwana Willybroad Alphonce amesema kuwa katika kufikia malengo na uendeshaji wameweza kutumia kiasi kikubwa cha fedha cha Zaidi ya Bilioni moja.

Na kuongeza kuwa, wakiwa miongoni mwa Watanzania wazawa, wamewaomba watanzania kuwaunga mkono kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamemsaidia mkulima aliyoko kijijini ambaye bidhaa zake zinaharibika huku mijini zikihitajika kwa wingi, kwani licha ya wao kuendesha shughuli za kilimo pia wamekuwa wakinunua baadhi ya mazai kutoka kwa wakulima wengine ikiwa tu na lengo la kusaidia soko hasa la ndani.

“ Wateja watakao fika dukani kwetu watajipatia vitu mbalimbali. Ni wakati muafaka sasa kuchangamkia fursa hii ya bidhaa za mashambani ambazo zinatoka kwenye ardhi yetu ya nyumbani yenye rutuba za kutosha na uhifadhi wa hali ya usafi na usalama kwa mlaji.

Tunawakaribisha wote wanaotambua umuhimu wa kupata lishe bora kupitia matunda na mboga mboga huku tukiwasisitiza wale wote wenye watoto kuhakikisha wanawaleta pale Farm Fresh Bar waanze kuzoea toka mapema kuchangamana katika Bar zenye manufaa Kiafya” alimalizia

Tomoni Farms Limited inaendesha duka hilo la kisasa la mazao ya shambani, pia ina mgahawa na Bar maalum ambayo inahudumia bidhaa za matunda pekee ikiwemo juice za kila aina pamoja na masuala yote ya vyakula vya mboga mboga ambavyo ni vya asili.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More