Thursday, June 9, 2016

JANGILI WA MENO YA TEMBO ASHUGHULIKIWA KISAWASAWA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, imemhukumu, Johnface Lyang’oka, mkazi wa Magozi, Pawaga wilayani Iringa; kifungo cha miaka 15 jela au kulipa faini ya Sh Bilioni 1.65 baada ya kupatikana na makosa mawili yaliyomuhusisha na biashara ya meno ya Tembo 34.

Lyang’oka alifikishwa mahakamani hapo pamoja na mtuhumiwa mwingine katika kesi hiyo, Halfani Balobani baada ya kukamatwa Julai 30, 2015 akituhumiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai 16 na 18, mwaka 2015.

Mahakama hiyo ilimuachia huru, Balobani aliyekuwa mshatakiwa  wa kwanza katika kesi hiyo iliyohusisha watuhumiwa wengine wanne ambao hawajakamatwa baada ya Lyang’oka aliyekuwa mshatakiwa wa pili kukana kumfahamu mtuhumiwa namba moja katika kesi hiyo.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Andrew Scout alisema; “Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa upande wa mashtaka dhidi ya washatakiwa hao.”

Alisema mahakama imemuona hana hatia Balobani baada ya mshatakiwa mwenza kukana kumfahamu na badala yake kuwataja watu wengine wanne ambao hawakufikishwa mahakamani hapo kwakuwa hawajakamatwa na Polisi ili waunganishwe katika kesi hiyo.

“Kwahiyo mahakama yangu imemtia hatiana kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa Johnface Lyang’oka na nina muhukumu kama ifuatavyo,” alisema.

Alisema katika shtaka la kwanza linalomuhusisha Lyang’oka na biashara ya meno ya Tembo kinyume na kifungu cha sheria 80(1) na 84(1) ya Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 inayokwenda sambamba na kifungu cha 14 (d) na kifungu cha 57 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002 anahukumiwa:

“Kwenda jela miaka 15 au faini ya Sh 1,548,000,000 baada ya kuuza meno ya Tembo 32 ambayo kwa wakati huo yalikuwa na Thamani ya Sh 516,000,000,” alisema hakimu huyo.

Alisema katika shtaka pa pili mtuhumiwa katika kipindi hicho hicho, alijihusisha na biashara ya meno ya Tembo mawili ambayo wakati huo yalikuwa na thamani ya Sh 32,250,000 kinyume na sheria hiyo.

Scout alisema kwa mujibu wa sheria hiyo ya wanyamapori, mtuhumiwa akikutwa na hatia anatakiwa kulipa mara tatu ya thamani ya meno ya Tembo kwa wakati huo, hivyo kwa makosa hayo mawili Lyang’oka anatakiwa kulipa faini ya jumla ya Sh 1,644,750,000 au jela miaka 15.

Mkuu wa wilayaya Iringa, Richard Kasesela aliizungumzia hukumu hiyo akisema itakuwa fundisho kwa majangili wengine wanaokamatwa ndani na nje ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha wakifanya ujangili.

Kasesela alikumbushia uamuzi wa serikali wa kuwataka wananchi wote wanaoingia kinyemela na kufanya shughuli zao za kimaendeleo katika eneo la Nyaluu, Pawaga ambalo ni eneo la hifadhi ya wanyamapori ya jamii kutokanyaga katika eneo hilo linalotumiwa na majangili kama mlango wa ujangili.

“Baada ya kutoke mafuriko na kubaini kuwepo na watu wanaofanya shughuli za kilimo katika eneo hilo na kuwepo kwa taarifa za baadhi yao kujihusisha na ujangili, serikali iliagiza watu wote katika eneo hilo waondoke. Narudia tena, kama bado wapo waondoke kabla mkono wa sheria haujawafikia,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More