DK.
Vincent Mashinji Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(chadema), amesema kuwa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi
ndiyo msingi imara pekee unaoweza kuweka mifumo na taasisi kwa ajili ya
maendeleo ya kweli yatakayogusa maslahi ya Watanzania wote badala ya
nchi kuongozwa na kauli za viongozi.
Kutokana
na umuhimu huo wa kuzingatia maoni ya wananchi yanayobeba matakwa yao
katika mchakato wa Katiba Mpya, amesema kuwa Chadema hakitashiriki kura
ya maoni ya Katiba Mpya Inayopendekezwa ambayo ilipitishwa na Bunge
Maalum la Katiba baada ya kubadili na kuondoa mapendekezo yaliyotolewa
na wananchi kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya.
Badala
yake, Chadema kitaendelea kuweka agenda ya kupigania Katiba Mpya na
bora katika vipaumbele vyake, kwa sababu itatibu vidonda na kumaliza
makovu yaliyoko katika jamii kutokana na matatizo mbalimbali kama vile
ukosefu wa haki, migogoro ya ardhi, wananchi kukosa huduma za msingi za
kijamii zikiwemo elimu, maji na afya.
Dkt.
Mashinji aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipoukaribisha
ujumbe wa Chama cha Centre Party cha Norway uliofika ofisini kwake
jijini Dar es Salaam kutia saini makubaliano ya ushirikiano kati ya
vyama hivyo kwenye Mradi wa Elimu ya Demokrasia awamu ya pili
unaofanyika Wilaya ya Mtwara Vijijini.
Dkt.
Mashinji pia amekishukuru chama hicho kwa kusaidia kutoa elimu ya uraia
kwa Watanzania hususani maeneo ya vijijini katika mradi ambao
unahusisha vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi ndani ya Bunge, huku
akisisitiza kuwa Chadema kiko tayari kwa ushirikiano unaozingatia
maslahi na matakwa ya wananchi hasa katika kukuza uelewa wa kudai haki,
demokrasia na uongozi bora ndani ya nchi.
“Suala
la Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi kama ilivyowasilishwa
kwenye rasimu ya pili na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ni agenda
muhimu kwa Watanzania wapenda nchi yao na sisi ni kipaumbele kwa mwaka
huu na kuendelea hadi hapo nchi yetu itakapopata Katiba Mpya ya
Wananchi.
“Jana
na leo tumewasikia baadhi ya viongozi wa serikali wakisema kuwa
wanajiandaa kuitisha kura ya maoni…hatutashiriki kura ya maoni ya Katiba
Mpya Inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba. Tunajua Watanzania
wengi wanataka Katiba Mpya iliyotokana na maoni yao, si ile
iliyochakachuliwa bungeni.
“Katiba
Mpya iliweka masuala kuhusu haki za wananchi, kuimarisha misingi na
kuweka mifumo ya demokrasia na uongozi bora, walau kwa kuanzia. Hatuwezi
kusema sasa tutatumia mikakati gani kuwahamasisha Watanzania kuidai
Katiba Mpya…tutajua namna ya kuvuka tukishafika mtoni,” Alisema
Aidha,
Katibu Mkuu Dkt. Mashinji alisisitiza kuwa suala la nchi kuwa na
misingi na mifumo imara ya demokrasia na uongozi bora ni muhimu kwa
Tanzania, katika wakati ambapo nchi inaelekea kwenye uchumi mkubwa wa
nishati ya gesi na mafuta, akisema vinginevyo ni hatari iwapo taifa
lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, litaendelea kuwa na wananchi
waliokata tamaa kutokana na mfumo mbovu uliopo.
Kwa
upande wake ujumbe huo uliokuwa ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Centre
Party, Knut Olsen, ulisema kuwa chama hicho kinashukuru kwa mradi huo
kuingia katika hatua ya pili kuanzia mwaka 2016-2019 huku hatua ya
kwanza ikiwa na mafanikio makubwa katika jamii ya wananchi wa maeneo ya
pembezoni.
“Kama
unavyojua, mradi huu kupitia TCD unahusisha vyama vyote vyenye
uwakilishi ndani ya bunge, na lengo letu ni kuwajengea uwezo viongozi wa
vyama hasa wanawake na vijana katika ngazi ya jamii kwenye vitongoji,
vijiji, kata na bunge ili waweze kushiriki mchakato wa maamuzi.
Tunatarajia kuendelea kupata ushirikiano katika hatua ya pili,” alisema Inger Bigum, ambaye ni Meneja wa Mradi hapa nchini.
Wengine
waliokuwa katika ujumbe huo wa Centre Party ni pamoja na Vijana Sara
Hamre Katibu Mkuu wa, Katibu Mkuu wa Wanawake, Eline Stokstad-Oslan na
Kristin Madsen Katibu Mkuu wa Wazee.
Mradi
huo wa Elimu ya Demokrasia katika Wilaya ya Mtwara Vijijini unaohusisha
vyama vyenye uwakilishi bungeni kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD) chini ya ufadhili wa chama hicho, katika awamu ya kwanza
ulihusisha kata za Msangamkuu, Nanyamba, Ziwani na Mbembaleo na katika
sasa awamu ya pili utakuwa katika kata za Mkunwa, Tangazo, Mayanga na
Madimbwa.